Apr 25, 2024 02:35 UTC
  • Kuiwekea vikwazo sekta ya ulinzi ya Iran, zawadi mpya iliyotunukiwa Israel na Magharibi

Katika hatua uliyochukua ili kuufurahisha utawala wa Kizayuni wa Israel, Umoja wa Ulaya umetangaza kuwa utapanua wigo wa vikwazo ulivyoiwekea sekta ya ulinzi ya Iran.

Siku chache baada ya hatua ya utiaji adabu ambayo haijawahi kushuhudiwa, iliyochukuliwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kushambulia kwa makombora na ndege zisizo na rubani vituo na maeneo ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu likiwa ni jibu kwa shambulio la kijinai lililofanywa na utawala huo dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria, Umoja wa Ulaya umetangaza kuwa unapanua wigo wa vikwazo vyake dhidi ya sekta ya ulinzi ya Iran.
Siku ya Jumatatu, Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya (EU), alithibitisha kupitishwa uamuzi huo wa kupanua vikwazo vya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya Iran, na kusisitiza kutofurahishwa Ulaya na shambulio la hivi karibuni la makombora na ndege zisizo na rubani lililofanywa Iran dhidi ya Israel. Borrell amedai kuwa lengo la vikwazo hivyo ni kuzuia kustawi na kupiga hatua zadi sekta za makombora na ndege zisizo na rubani za nchi kama Iran na Russia.
Josep Borrell

Siku chache zilizopita, serikali za Marekani na Uingereza ziliwawekea vikwazo watu 16 na taasisi 13 za Iran kwa visingizio hewa zilivyotoa dhidi ya Iran. Wiki iliyopita, Jake Sullivan, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani alizungumzia hatua za nchi yake zenye lengo la kuziwekea vikwazo vipya sekta za makombora na ndege zisizo na rubani za Iran akisema, Washington inatarajia washirika wake pia kufuata hatua hiyo.

Kwa msingi huo na kama ilivyotarajiwa, muda mfupi baada ya wito huo wa Marekani, Umoja wa Ulaya ulitangaza kuwa utaiwekea vikwazo sekta ya ulinzi ya Iran, hususan sekta ya makombora na ndege zisizo na rubani. Kwa hakika inashangaza kwamba, badala ya Umoja wa Ulaya kujaribu kukomesha jinai za Israel huko Ghaza na vitendo vyake vya kichochezi katika eneo, umeamua kuiwekea vikwazo sekta ya ulinzi ya Iran, ili kuonyesha uungaji mkono wa kila hali kwa utawala huo muuaji na mfanya mauaji ya kimbari, hatua ambayo imepokewa kwa mikono miwili na waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni Israel Katz.
Hatua mpya ya nchi za Magharibi ya kuiwekea vikwazo sekta ya ulinzi ya Iran imekuja baada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kufyatua makumi ya makombora na ndege zisizo na rubani kulenga miundombinu ya kijeshi na kiusalama ya utawala wa Kizayuni mnamo alfajiri ya kuamkia Jumapili ya tarehe 14 Aprili. Operesheni hiyo iliyopewa jina la "Ahadi ya Kweli" ilitekelezwa katika fremu ya kanuni ya Uhalali wa Kujihami kwa mujibu wa Kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa, kujibu shambulizi la anga la Aprili Mosi lililofanywa na utawala wa Israel dhidi ya jengo la ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Damascus, lililopelekea kuuawa shahidi makamanda na washauri saba wa kijeshi wa Iran.

Hatua za Marekani na Ulaya za kuamua kuziwekea vikwazo sekta za makombora na ndege zisizo na rubani za Iran zinafanyika wakati huu, ambapo kimsingi Jamhuri ya Kiislamu inajaribu kustawisha zaidi uwezo wake wa kiulinzi katika sekta zote, hususan makombora na ndege zisizo na rubani, ambazo msingi wa matumizi yake ni wa kiulinzi na kujihami ulioasisiwa kwa kutegemea wataalamu wa ndani kwa ajili ya kuzuia hujuma na uvamizi; na kwa hivyo hatua za vikwazo za Magharibi, kama ilivyothibitika huko nyuma, hazitaweza kuzuia maendeleo ya Iran ya uwezo wa kujihami.

Kwa maana hiyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kama ilivyo nchi nyingine yoyote, ina haki ya kuchagua nyenzo itakazo za kiulinzi kulingana na sheria za kimataifa.
Kuimarishwa uwezo wa makombora na wa ndege zisizo na rubani wa Iran nao pia unafanywa kukidhi mahitaji ya Uhalali wa Kujihami na kuandaa mazingira ya kutekeleza kanuni ya "Kujilinda" kwa mujibu wa Kifungu cha 51 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Kuhusiana na hilo, vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kufuata msingi wa majukumu yake, vimeazimia kwa dhati kutekeleza mkakati wa kuimarisha uwezo wa zana na silaha; na hatua zinazozidi kupigwa siku baada ya siku katika uga wa uundaji na uzalishaji wa kila aina ya makombora ya kruzi na balestiki pamoja na droni za utoaji mafunzo, za upelelezi na za mashambulizi ni matunda ya juhudi hizo ambazo zimewezesha kusambaratishwa mfumo wa ulinzi wa anga wa adui.../

Tags