Apr 25, 2024 03:21 UTC
  • Iran yaitaka UN kukomesha mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza

Mwakilishi wa Iran katika ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva amemwandikia barua mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, akiwaomba kuchukua hatua za haraka za kukomesha mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya watu wa Gaza huko Palestina.

Katika barua tofauti alizowaandikia mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Ali Bahraini, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Geneva, ameorodhesha jinai za kivita, jinai dhidi ya binadamu na mauaji ya halaiki yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza na kuandika kuwa: Ukatili unaofanywa na Israel katika eneo hilo haumshangazi mtu yeyote tena; mauaji haya ya kimbari yanapaswa kukomeshwa haraka iwezekanavyo.

Akiashiria ripoti ya Taasisi ya Ulinzi wa Raia huko Gaza kuhusu kugunduliwa  kaburi la umati la mamia ya mashahidi wa Kipalestina waliouawa na kuzikwa na wanajeshi wa Israel katika eneo la Nasser Medical Complex huko Khan Yunis, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran mjini Geneva amesema: Ukweli huu unaonyesha kwamba iwapo uhalifu huu wa kutisha hautakomeshwa mara moja, bila shaka tutashuhudia kurudiwa kwa majanga kama haya.

Kaburi la umati la Wapalestina waliouawa na kuzikwa na jeshi la Israel

Katika barua hizo, Bahraini amenukuu vipengee vya sheria za kimataifa, kama vile mikataba ya Geneva na kusema, kushambulia hospitali na vituo vya matibabu, kutumia njaa kama silaha ya vita, kuzuia misaada ya kibinadamu na kadhalika ni mifano ya uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita.

Wakati huo huo, Chuo Kikuu cha Al-Azhar nchini Misri kimetoa taarifa kikilaani jinai za kutisha zinazofanywa na Israel dhidi ya wanawake, watoto na wazee katika Ukanda wa Gaza, ya karibuni zaidi ikiwa ni kugunduliwa makaburi ya umati katika maeneo ya Hospitali za Al-Nasser na Al-Shifa.

Tags