May 23, 2024 13:44 UTC
  • Watu milioni 3 washiriki mazishi ya Rais Ebrahim Raisi mjini Mashhad

Waombolezaji zaidi ya milioni tatu wameshiriki katika mazishi ya kumuaga na Rais Ebrahim Raisi wa Iran, aliyekufa shahidi katika ajali ya helikopta iliyotokea Jumapili iliyopita katika mkoa wa Azarbaijan Mashariki, kaskazini magharibi mwa Iran.

Marehemu Sayyid Raisi anazikwa usiku huu katika chumba cha Dar al-Salam katika Haram tukufu ya Imam Ridha AS,  Imam wa Nane wa Waislamu wa Kishia, iliyoko katika mji mtakatifu wa Mashhad ulioko kaskazini mwa Iran.

Ndege iliyokuwa imebeba mwili wa Shahidi Raisi iliwasili adhuhuri ya leo katika Uwanja wa Ndege wa Hasheminejad mjini Mashhad na kupokewa na viongozi mbali mbali wa kisiasa na kidini wa Jamhuri ya Kiislamu.

Aidha vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa vimeonyesha mijumiko ya mamilioni ya wakazi wa mji huo mtukufu waliojitokeza mabarabarani na katika uwanja wa ndege kuusindikiza na kuuaga mwili wa Sayyid Raisi.

Mapema leo, miili ya Raisi na wenzake ilipokewa na kuagwa na wakazi wa mji wa Birjand, makao makuu ya mkoa wa Khorasan Kusini, ambako mwezi Machi mwaka huu alichaguliwa kuwa mwakilishi wa mkoa huo wa mashariki katika uchaguzi wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaochagua na kusimama kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Jana Jumatano, mamilioni ya watu walishiriki katika mazishi ya kuwaaga mashahidi Rais Sayyid Ebrahim Raisi, Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mashahidi wenzao wengine hapa mjini Tehran.

Wakazi wa Mashhad wakiuaga mwili wa Sayyid Raisi

Helikopta iliyokuwa imembeba Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jumapili jioni Mei 19, 2024 ilipata ajali ilipokuwa ikirejea kutoka kwenye hafla ya ufunguzi wa bwawa la Qiz Qalasi kwenye mpaka wa pamoja wa Iran na Jamhuri ya Azerbaijan.

Wakati helikopta hiyo ilipokuwa inaelekea mji wa Tabriz, ilianguka katika eneo la Varzghan mkoani Azarbaijan Mashariki, kaskazini-magharibi mwa Iran. Ndani yake walikuwemo pia Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje, Imam wa Ijumaa wa Tabriz, Gavana wa Azarbaijan Mashariki na watu wengine; na wote pamoja wakaifika hadhi tukufu ya kufa shahidi.

Risala za rambirambi zimekuwa zikimiminika Iran kutoka duniani kote, huku nchi kama Syria, Lebanon, Iraq, India, Pakistan, Tajikistan, Uturuki, Cuba na Sri Lanka zikitangaza maombolezo ya kitaifa.

Tags