May 24, 2024 07:26 UTC
  • Makamanda wa IRGC na wakuu wa kambi ya muqawama wakutana Tehran

Makamanda waandamizi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) wamekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa makundi ya muqawama waliokuja hapa nchini Iran kushiriki mazishi ya viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu akiwemo Rais Ebrahim Raisi waliokufa shahidi katika ajali ya helikopta Jumapili iliyopita.

Mkutano huo uliofanyika jana Alkhamisi hapa Tehran umejadili matukio ya sasa ya kijeshi, kisiasa na kijamii katika Ukanda wa Gaza, Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa dhidi ya Wazayuni na nafasi ya mrengo wa muqawama katika eneo. Washiriki wa mkutano huo wamesisitizia haja ya kuendeleza mapambano na muqawama hadi pale Wapalestina watakapopata ushindi kamili dhidi ya Wazayuni katika Ukanda wa Gaza.

Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC), Brigedia Jenerali Esmaeil Qaani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha jeshi la SEPAH, Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na Sheikh Naim Qassim, Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ni miongoni mwa viongozi wa Iran na kambi ya muqawama walioshiriki mkutano huo.

Kiongozi Muadhamu katika mazungumzo na Ismail Haniya mjini Tehran

Juzi Jumatano pia, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza katika mazungumzo na Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas na ujumbe alioandamana nao kwamba, ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kutokomezwa utawala wa Kizayuni na kupata ushindi Palestina itatimia.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kuwa itafanya kila iwezalo katika kuwatetea wananchi madhulumu wa Palestina na mapambano halali ya muqawama dhidi ya Wazayuni, na kukomeshwa jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya taifa la Palestina.

Tags