Jun 24, 2024 06:49 UTC
  • Umuhimu wa safari za kampeni za wagombea wa uchaguzi wa rais wa Iran

Siku ya Jumamosi, mikutano ya kampeni za uchaguzi za wagombea wa muhula wa 14 wa uchaguzi wa rais wa Iran ilifanyika katika miji tofauti humu nchini na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya wananchi.

Kati ya wagombea sita wa uchaguzi wa urais, wagombea watatu, "Mohammed Baqer Qalibaf," "Saeed Jalili" na "Masoud Mezikian" walifanya mikutano ya hadhara na wafuasi wao katika miji kadhaa tofauti na pia kusikiliza maoni, kutangaza sera na mipango yao iwapo wataingia madarakani. Siku hiyo ya Jumamosi pia, wagombea wengine watatu, Alireza Zakani, Sayyid Mohsen Ghazizadeh Hashemi na Sheikh Mustafa Pourmohammadi nao pia walitangaza sera zao.

Kufanyika mikusanyiko mikubwa ya kampeni za uchaguzi katika miji mbalimbali ya Iran ikiwa ni pamoja na miji ya Tehran, Sanandaj, Isfahan, Shiraz, Qazvin, Ahvaz na Isfahan ni ushahidi wa wazi kwamba midahalo baina ya wagombea iliyoitishwa na Shirika la Redio na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imevutia hisia za watu wengi kushiriki mikutano ya hadhara ya wagombea wakiwa na hamasa kubwa. Hii ni ishara kuwa ushiriki wa wapiga kura nao utaongezeka na utakuwa mkubwa hapo tarehe 28 Juni. 

Wagombea urais wa duru ya 14 ya uchaguzi wa Rais wa Iran

 

Hatua ya wagombea wa urais kutembelea miji tofauti na kukutana na wafuasi wao bila ya shaka yoyote kama tulivyosema, itakuwa na taathira ya moja kwa moja katika idadi ya wapiga kura na kushiriki kwa wingi wananchi kwenye uchaguzi huo. Wagombea wa uchaguzi huo wanaweza kutumia fursa ya siku zilizobakia kutangaza vizuri sera zao na kuongeza idadi ya kura zao. Mirengo tofauti ya kisiasa ya Iran, kila mmoja una mgombea wake katika uchaguzi huo na aina hii ya wagombea itakuwa ni chachu ya kuongezeka idadi ya watu watakaojitokeza kwenye uchaguzi huo.

Jambo jingine kuu na muhimu ni umakini wa wagombea katika kuchunga kanuni za maadili ya midahalo na mikusanyiko ya uchaguzi, jambo ambalo linaweza kuimarisha umoja na mafungamano ya ndani na kuvunja njama za maadui, ambazo lengo lake kuu litakuwa ni kuwakatisha tamaa wananchi kupitia uchaguzi huo. Kwa kweli, malengo haya machafu ya maadui hayatafanikiwa iwapo watu na hasa wagombea, watachunga maadili kama kawaida.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, siku ya Jumamosi wakati alipoonana na maafisa wa Idara ya Mahakama, alivitaja vipindi vya televisheni vya uchaguzi kuwa vinaendeshwa vizuri kwa ajili ya kuwafahamisha wananchi mitazamo tofauti ya wagombea. Hapo hapo lake alitahadharisha kwamba, mijadala ya wagombea kwenye Televisheni au kauli zao nyingine zisipelekee kutoa matamshi ya kumfurahisha adui kwa ajili tu ya kuwashinda wapinzani wao katika uchaguzi. 

Uchaguzi nchini Iran

 

Aliongeza kuwa: Tunavyoamini ni kwamba, wagombea wote wanaipenda Iran na Jamhuri ya Kiislamu. Kwa sababu wote wanataka kuwa rais ili kuhudumia wananchi ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Hivyo wanapaswa kuwa makini sana katika matamshi yao na wajiepushe kabisa kumfurahisha adui.

Kuwepo wagombea wa mirengo tofauti katika uchaguzi wa urais kuna umuhimu mkubwa kati ya wananchi. Kwa upande mwingine, mtazamo wa wananchi kwa wagombea wa uchaguzi wa rais nako kuna taathira ya moja kwa moja katika kujitokeza kwa wingi wananchi kwenye upigaji kura. 

Hali iliyojitokeza hivi sasa baada ya duru tatu za midahalo baina ya wagombea urais ikiwa imebakia mijadala na midahalo mingine miwili, inaonesha shauku kubwa ya wananchi kushiriki katika uchaguzi wa urais. Uchaguzi huo unatarajiwa kuwa wa hamasa zaidi kuliko chaguzi za huko nyuma kama ambavyo unatarajiwa pia kuimarisha uhusiano wa kudumu kati ya makundi na mirengo mbalimbali ya wananchi na ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tags