Aug 11, 2024 07:35 UTC
  • Iran: Hatutaruhusu Israel ichochee moto wa vita Asia Magharibi

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inafanya hima kuzuia utawala wa Kizayuni wa Israel utimize ndoto yake ya kuwasha na kuchochea moto wa vita vya pande zote katika eneo la Asia Magharibi.

Ali Bagheri Kani amesema hayo leo Jumapili katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X na kusisitiza kuwa, "Tunaamini kuwa, utawala haramu wa Israel utapata ujasiri wa kuendelea kutenda jinai katika eneo iwapo hautaadhibiwa."

Kani ameeleza bayana kuwa, mataifa ya Kiislamu yanapasa kufanya jitihada za pamoja za kukomesha mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala katili wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amebainisha kuwa: Kwa kushadidisha mauaji ya kimbari dhidi ya raia, wakiwemo wanawake na watoto wadogo, utawala wa Kizayuni umeweka rekodi mpya ya ukatili katika jamii (ya kimataifa) ya wanadamu.

Miili ya Wapalestina waliouawa shahidi katika shule ya Tabieen

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria ukatili wa karibuni wa utawala wa Kizayuni ulioua shahidi Wapalestina zaidi ya 100 katika shule ya al-Tabieen inayohifadhi wakimbizi wa Kipalestina mashariki mwa jiji la Gaza na kueleza kuwa, undumakuwili wa Wamagharibi umeipa Israel uthubutu wa kuendelea kufanya jinai na vitendo vya kigaidi.

"Undumakuwili na unafiki wa Magharibi haupasi kupuuzwa. Serikali za Magharibi zinafumbia macho jinai za utawala wa Kizayuni, na hata zinaukingia kifua na kuupa himaya katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa," ameongeza Bagheri Kani.

 

Tags