Pezeshkian: Waislamu lazima waungane kukomesha jinai za Israel
(last modified 2024-08-27T02:35:23+00:00 )
Aug 27, 2024 02:35 UTC
  • Pezeshkian: Waislamu lazima waungane kukomesha jinai za Israel

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema kuna haja kwa mataifa ya Waislamu pamoja na nchi nyingine duniani kuungana na kuwa na sauti moja katika kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel na waungaji mkono wake kukomesha mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

Rais Pezeshkian alisema hayo jana Jumatatu hapa mjini Tehran katika mazungumzo yake na Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar.

Dakta Pezeshkian amesema anatumai kuwa, nchi za Kiislamu na mataifa mengine yanayoheshimu kanuni na taratibu za kimataifa, yatasimama pamoja na kuwashawishi 'walezi' wa utawala wa Kizayuni kuacha kuunga mkono utawala huo na kukomesha jinai na mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

Utawala katili wa Israel umewaua shahidi zaidi ya Wapalestina 40,400 katika Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7 mwaka jana 2023 hadi sasa, mkabala wa kimya cha taasisi za kimataifa kama Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Waziri Mkuu wa Qatar awali alikutana na Waziri mpya wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi 

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Qatar amempa Rais wa Iran salamu kutoka kwa Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, akibainisha kwamba Amir anatilia maanani umuhimu wa kuimarisha uhusiano na Iran.

Sanjari na kukosoa misimamo inayokinzana ya jamii ya kimataifa na wale wanaojiita watetezi wa haki za binadamu dhidi ya muathiriwa na mtenda jinai jinai huko Gaza, mwanadiplomasia huyo wa Qatar amesema kuwa, Doha itaendelea na juhudi zake za kusimamisha mapigano huko Gaza; na inatambua jukumu athirifu la Iran, mhusika mkuu katika suala hili.

Tags