Safari ya Mohammad Eslam mjini Vienna inayolenga kubainisha pande tofauti za mpango wa amani wa nyuklia wa Iran
Mohammad Eslami, Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekwenda Vienna Austria kushiriki katika mkutano mkuu wa mwaka wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kwa lengo la kufafanua pande tofauti za mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani.
Mohammad Eslami huku akiongoza ujumbe wa maafisa wa taasisi hiyo alielekea Austria siku ya Jumamosi tarehe 14 Septemba, kwa shabaha ya kushiriki katika mkutano wa 68 wa kila mwaka wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki. Jumatatu tarehe 16 Septemba, Makamu huyo wa Rais amepangiwa kutoa hotuba katika Mkutano Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki. Mohammad Eslami atakutana na Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na pia kufanya mikutano ya pande mbili na viongozi wenzake wa taasisi za nyuklia wa baadhi ya nchi kwa lengo la kubadilishana uzoefu na masuala yanayohusiana na sekta ya nyuklia.
Kwa mnasaba wa kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran, katika sehemu ya matukio ya pembeni ya Mkutano wa 68 wa Baraza Kuu la Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, wataalamu wa sekta ya nyuklia ya Iran watazungumza na kuwasilisha uzoefu, nafanikio na uwezo wao katika uwanja wa ujenzi wa mitambo ya nyuklia, vinu vya utafiti, mzunguko wa fueli, teknolojia ya matumizi ya mionzi, isotopu thabiti na mafunzo maalum kwa wafanyakazi wa sekta hiyo.
Katika maonyesho yatakayofanyika kando ya mkutano huo, uwezo wa sekta ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikiwa ni pamoja na nyanja mbalimbali za uchunguzi wa roboti, utumiaji wa roboti katika tasnia ya nyuklia, uzalishaji wa nishati safi na endelevu, bidhaa za radiopharmaceuticals, mifumo ya vipimo vya nyuklia na uwezo wa Iran katika uwanja wa maendeleo ya teknolojia ya plasma viwandani, mazingira, matibabu na afya, usalama wa chakula pamoja na hatua zinazochukuliwa katika uwanja wa taka za nyuklia utaonyeshwa kwa wageni watakaotembelea maonyesho hayo.
Mkutano wa 68 wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki unafanyika huko Vienna, mji mkuu wa Austria kuanzia leo Jumatatu tarehe 16 hadi 20 Septemba. Mkutano huo ni mojawapo ya vitengo vikuu vya kubuni sera za wakala huo, ambapo unajumuisha nchi zote wanachama. Hufanyika kila mwaka mwezi Septemba katika makao makuu ya Shirika hilo mjini Vienna ambapo maafisa wa ngazi za juu na wawakilishi wa nchi wanachama hujadili masuala muhimu ya nyuklia.
Wataalamu na wanasayansi vijana wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika miaka ya hivi karibuni na licha ya vikwazo na vizingiti wanavyowekewa njiani na Marekani na washirika wake wa Magharibi, wamepata mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali za nyuklia, mafanikio ambayo yameakisiwa na vyombo vya habari vya Magharibi na kuwashangaza wataalam wa Marekani na Ulaya, jambo ambalo limewafanya kutambua na kuheshimu uwezo wa vijana wa Iran hasa katika sekta ya tiba ya nyuklia.
Pamoja na hayo, mwenendo huo wa chuki na uadui haujasimamisha maendeleo ya Iran katika sekta ya nyuklia, ambapo wataalamu wa Iran licha ya kukabiliwa na vikwazo na matatizo chungu nzima katika uwanja huo kutoka nchi za Magharibi, wamefanikiwa kuboresha nafasi ya nchi katika sekta ya teknolojia ya nyuklia, jambo ambalo limeifanya Iran leo kuchukuliwa katika eneo na kimataifa kuwa soko muhimu la bidhaa za nyuklia.
Uwepo wa Mohammed Eslami, Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran huko mjini Vienna Austria na kufafanuliwa malengo ya mpango wa nyuklia wa Iran, mbali na kuonyesha mafanikio ya nyuklia ya Iran pembeni mwa kikao hicho bila shaka kutapunguza propaganda za uwongo na za chuki za vyombo vya habari vya Magharibi dhidi ya Iran, na wakati huo huo kuandaa uwanja unaofaa kwa ajili ya ushirikiano mpana zaidi kati ya Iran na nchi mbalimbali za dunia katika sekta ya nyuklia.
Suala jingine muhimu, ni sisitizo la Jamhuri ya Kiislamu la udharura wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kuzingatia hatua za kuibua mivutano na uharibifu zinazofanywa na utawala haramu wa Israel unaohesabika kuwa tishio la nyuklia kwa eneo, katika kivuli cha uungaji mkono wa Marekani na kimya cha nchi za Magharibi. Utawala huo hauheshimu sheria zozote za wakala huo, ambapo kuna ripoti za kuaminika zinazothibitisha kwamba jeshi la utawala huo limetumia mabomu hatari yenye uranium iliyohafifishwa katika vita vyake vya mauaji ya umati huko Ukanda wa Gaza.