Pezeshkian: Iran haijali nani ameshinda uchaguzi wa rais Marekani
(last modified Fri, 08 Nov 2024 02:37:54 GMT )
Nov 08, 2024 02:37 UTC
  • Pezeshkian: Iran haijali nani ameshinda uchaguzi wa rais Marekani

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Haijalishi kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nani ameshinda uchaguzi wa rais nchini Marekani.

Rais  Masoud Pezeshkian amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni taifa lenye heshima na adhimu linaloegemea kwenye nguvu zake za ndani. Amesema, kwa Iran hakuna tofauti nani ameshinda uchaguzi wa rais huko Marekani, kwa sababu Iran na muundo wa Jamhuri ya Kiislamu unategemea nguvu zake za ndani.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa, Iran haitakuwa na fikra funge na finyu katika kuendeleza uhusiano wake na nchi nyingine na amesisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu inalipa kipaumbele suala la kupanua uhusiano wake na nchi za Kiislamu na majirani zake na inaamini kwa dhati katika suala la kuimarishwa umoja na mshikamano baina ya mataifa ya Kiislamu.

Pezeshkian amefafanua kuwa: Lau nchi zote za Ulimwengu wa Kiislamu zingeimarisha udugu na kuwa na umoja na mshikamano, utawala wa Kizayuni wa Israel usingethubutu kuwaua watu madhulumu wa Palestina na Lebanon kama inavyoshuhudiwa hivi sasa.