Araqchi: Tupo tayari kwa mazungumzo yenye tija kuhusu mpango wetu wa nyuklia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Tehran iko tayari kufanya mazungumzo yenye tija na bila ya kuchelewa kuhusu mpango wake wa nyuklia.
Sayyid Abbas Araqchi alisema jana usiku katika mahojiano maalumu na televisheni ya CCTV ya China kwamba: "Kwa zaidi ya miaka miwili tumefanya mazungumzo kwa nia njema na nchi za kundi la 5+1 na mwishowe tukafikia makubaliano ambayo yalipongezwa na dunia nzima kama mafanikio ya diplomasia; Hata hivyo Marekani iliamua kujitoa katika makubaliano hayo bila sababu yoyote na kuifikisha hali ya mambo hapa tulipo.
Araqchi amekumbusha kuwa, kwa mtazamo wa Iran, muundo uliopo kwa sasa ni sawa na ule ya zamani ya JCPOA, yaani kujenga hali ya kuaminiana kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran mkabala wa kuondolewa vikwazo na kuongeza kuwa: Tulifanya duru moja ya mazungumzo na nchi za Ulaya na duru ya pili ya mazungumzo tayari imeainishwa ambapo katika muda wa chini ya wiki mbili zijazo Tehran itafanya mazungumzo na nchi tatu za Ulaya yaani Ujerumani, Ufaransa na Uingereza.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema pia kuhusu Marekani kwamba: Ni kawaida kwamba serikali mpya ya nchi hiyo inapasa kubuni sera zake; na Iran pia itafanya uamuzi kulingana na sera hizo. China na Russia pia zinapasa kuendeleza mchango wao mkuu katika mazungumzo hayo na hili ni takwa na irada ya Iran.