Waitifaki wa Trump: Maajenti wa Mossad wanajaribu kuvuruga mazungumzo ya Iran na Marekani
(last modified Wed, 30 Apr 2025 11:55:07 GMT )
Apr 30, 2025 11:55 UTC
  •  Waitifaki wa Trump: Maajenti wa Mossad wanajaribu kuvuruga mazungumzo ya Iran na Marekani

Vyombo vya habari na wafuasi wa karibu na Rais Donald Trump wa Marekani wamesema kuwa mawakala wa Mossad na wapenda vita wanaisukuma Marekani katika mzozo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tucker Carlson muendeshaji  mhafidhina wa kipindi cha mazungumzo cha "Tucker Carlson Tonight" wiki iliyopita alikuwa mwenyeji wa afisa wa ngazi ya juu wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) ambaye alidai kuwa alifutwa kazi kwa sababu alionekana kuwa kikwazo kwa hatua za uhasama za Marekani dhidi ya Iran.

Dan Caldwell ambaye alikuwa mshauri wa ngazi ya juu wa Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, alifutwa kazi mapema mwezi huu kwa madai kwamba alivujisha habari za siri kuhusu mazungumzo yaliyofanywa na  Hegseth katika mtandao wa kijamii wa Signal.

Jumapili wiki hii pia, mtangazaji mwingine wa kihafidhina, Clayton Morris ambaye ni mtangazaji wa zamani wa Fox News alisema: Sauti za kuiunga mkono Israel zilikuwa zikifanya kazi kwa muda wa ziada ili kusambaratisha timu ya watendaji wanaopinga vita iliyowekwa na Trump katika Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon). 

Mtangazaji huyo wa kihafidhina anasema: "Tumejifunza hapa  kwamba maajenti wa zamani wa shirika la ujasusi la Israel (Mossad) wanafanya kazi kwa muda wa ziada kwenye mitandao ya kijamii na kwa njia ya siri wakijaribu kumdhoofisha Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth.

Utawala wa Trump umegawanyika kati ya wahafidhina vindakindaki kama Marco Rubio Waziri wa Mashauri ya Kigeni, na Mike Waltz Mshauri wa Usalama wa Taifa kwa upande mmoja; na wale wanaosimamia kauli mbiu ya "Marekani Kwanza" kama vile Mkuu wa Wafanayakazi wa White House, Susie Wiles na Tulsi Gabbard Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa.