Araghchi: Iran imeazimia kikweli kufikia makubaliano yenye uwiano
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amesema kuwa Iran hivi sasa imeazimia kikwelikweli kufikia makubaliano ya haki na yenye uwiano kuliko wakati mwingine wowote.
"Sisi, pamoja na pande za Oman na Marekani, tuliamua kuakhirisha duru ya nne ya mazungumzo kwa sababu za kilojistiki na kiufundi," ameandika Araghchi katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X.
Ameongeza kuwa, kwa upande wa Iran, hakuna mabadiliko yoyote katika dhamira yetu ya kufikia makubaliano ya haki.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema:' Tumedhamiria vilivyo hivi sasa kufikia makubaliano ya haki na yenye uwiano ambayo yatahakikisha vikwazo vinakomeshwa na kujenga hali ya kuaminiana ya kwamba miradi ya nyuklia ya Iran itaendelea kuwa ya amani siku zote kwa sharti makubaliano hayo yatoe dhamana ya kuheshimiwa kikamilifu haki za Iran.
Jana Alkhamisi Ismael Baqhaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alitangaza mabadiliko ya tarehe ya duru ijayo ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani ambayo yalipangwa kufanyika Jumamosi Mei 3 huko Roma, Italia.
Baghaei, amesisitizia tena irada na azma ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kutumia diplomasia kudhamini maslahi halali na ya kisheria ya wananchi wa Iran na kukomesha vikwazo na mashinikizo ya kiuchumi ambayo yanakanyaga haki za binadamu na ustawi wa kila Muirani.