Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran: Iran haitaachana na haki yake ya teknolojia ya nyuklia
(last modified Fri, 23 May 2025 12:13:16 GMT )
May 23, 2025 12:13 UTC
  • Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran: Iran haitaachana na haki yake ya teknolojia ya nyuklia

Imam wa muda wa Swala ya Ijumaa hapa Tehran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitasalimu amri na kuachana na haki yake isiyoweza kupokonywa ya matumizi ya amani ya teknolojia ya nyuklia.

Akihutubia khutba za Swala ya Ijumaa ya leo hapa mjini Tehran, Hujjat al-Islam Kazem Sedighi amesisitiza kuwa, Tehran haitaacha msimamo wake kuhusu kuhifadhi haki ya kurutubishwa urani katika mazungumzo ya nyuklia.

Akirejelea mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya Iran na Marekani kuhusu suala la nyuklia, amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikipambana na madola yenye nguvu za nyuklia tangu mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, na katika kipindi chote cha miaka minane ya vita vya Kujihami Kutakatifu (vilivyoanzisha na Iraq dhidi ya Iran mwaka 1980-1988), na haijawahi kuachana na haki zake za msingi na kulinda maslahi ya taifa.

Amesema kuwa serikali ya Marekani ilitaka kuzungumzia masuala mbalimbali, lakini watoa maamuzi wa utawala wa Kiislamu waliafiki suala moja tu, ambalo lilikuwa suala la nyuklia.

"Leo, tasnia ya nyuklia imekuwa ya asili nchini Iran," mwanachuoni huyo amebainisha, akisisitiza kwamba, hakuna nafasi ya mazungumzo hata kidogo ikiwa wanataka kulipokonya taifa hili teknolojia ya nyuklia.

Kwingineko katika matamshi yake, Khatibu huyo Swala ya Ijumaa amelaani hujuma za kutisha za Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza.

Huku akizikemea nchi za Magharibi kwa kimya chao mkabala wa jinai hizo, Hujjat al-Islam Kazem Sedighi amewataka Wamagharibi kukata uhusiano wao na utawala dhalimu wa Kizayuni.