Pakistan yasisitiza uungaji mkono wa nchi hiyo kwa Iran
(last modified Sat, 05 Jul 2025 04:15:31 GMT )
Jul 05, 2025 04:15 UTC
  • Pakistan yasisitiza uungaji mkono wa nchi hiyo kwa Iran

Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, amesisitiza uungaji mkono usioyumba wa nchi yake kwa umoja wa ardhi na mamlaka ya kujitawala ya Iran.

Sharif ameeleza haya pambizoni mwa Mkutano wa 17 wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi (ECO) huko Khankendi, Azerbaijan. 

Waziri Mkuu wa Pakistan amesisitiza mshikamano na uungaji mkono usioyumba wa nchi yake kwa Tehran na amesifu msimamo na nafasi ya Rais Pezeshkian wakati wa vita vya 12 vilivyoanzisha na Israel dhidi ya Iran.

Katika mazungumzo hayo, viongozi wa Iran na Pakistan pia wamejadili ushirikiano wa nchi mbili katika nyanja zote na kueleza kuridhishwa kwao na mchakato wa maamuzi yaliyochukuliwa katika mkutano uliopita kwa shabaha ya kustawisha uhusiano wa pande mbili. 

Vilevile Rais wa Iran na Waziri Mkuu wa Pakistan wamejadili hali ya eneo la Asia Magharibi kufuatia vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran. 

Waziri Mkuu wa Pakistan ameipongeza Iran kwa kuulazimisha utawala wa Kizayuni kutangaza usitishaji vita katika uvamizi wake wa karibuni. 

Amesema Islamabad imedhamiria kuendelea kushirikiana kwa karibu na Tehran ili kudumisha amani katika kanda hii kupitia mazungumzo na diplomasia. 

Naye Rais Masoud Pezeshkian ameshukuru uungaji mkono mkubwa wa kidiplomasia wa Pakistan kwa Iran wakati wa vita vya hivi karibuni katika majukwaa ya kimataifa na kumshukuru Sharif kwa mchango muhimu wa Pakistan katika kupunguza hali ya mvutano.