Tuhuma dhidi ya Iran zaendelea licha ya Grossi kukiri tena kwamba Iran haitengenezi silaha za nyuklia
-
Rafael Grossi
Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) amesisitiza kuwa, hakuna ushahidi wa kuaminika kwamba Iran imepata silaha za nyuklia na kusisitiza ulazima wa kutatuliwa kidiplomasia suala la nyuklia la Iran.
Grossi ameeleza bayana kuwa, “Katika ripoti tuliyotayarisha kabla ya kuanza kwa vita hivyo vya siku 12, tulionya kuwa Iran haikuwa ikitoa taarifa za shughuli nyingi zinazohusiana na mpango wake wa nyuklia lakini, hatukuwa na ushahidi wa kuaminika kwamba Wairani wanamiliki silaha za nyuklia.
Aidha amesema kuhusu madai ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwamba utengenezaji wa Iran wa bomu la nyuklia ni suala la wiki chache tu, kwamba: "Iwapo Iran inaweza kuwa na silaha za nyuklia na iwapo inazo kweli ni masuala mawili tofauti kabisa."
"Takwimu tulizotoa kwa hakika zilikuwa nyeti kwa sababu zilionyesha aina ya uwezekano wa kutengeneza bomu la atomiki. Lakini hiyo haimaanishi kwa vyovyote kwamba uwezo huu ungetumika."
Alipoulizwa kwamba, itachukua muda gani mpaka Iran kutengeneza bomu la nyuklia kutokana na uwezo wake wa kabla ya vita, kama ingefanya hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA alieleza: "Kwanza, Wairani watalazimika kubadili urani iliyorutubishwa kuwa metali, kazi ambayo bado hawajaianza."
"Pili, inabidi watengeneze seti ya mifumo tata, kama vile kilipuzi, ambapo wakati huo huo inapaswa kuwa ndogo na ya kutosha kuingia kwenye kichwa cha nyuklia. Ndio maana nchi ambazo zimeunda silaha za nyuklia zimejaribu hilo kila mara."

Hii si mara ya kwanza, ya pili wala ya tatu ambapo Grossi ambaye misimamo na vitendo vyake vinawiana kikamilifu na matakwa na maslahi ya Israel na Marekani amesisitiza kuwa, hakuna nyaraka au ushahidi wa kuaminika kwamba Iran imefanikiwa kutengeneza silaha ya nyuklia.
Pamoja na hayo, madai ya mara kwa mara ya viongozi wa Israel na Marekani yamekuwa kwamba Iran inajaribu kutengeneza silaha za nyuklia na kwamba imekaribia kufikia hilo. Hiki kimsingi kilikuwa kisingizio cha utawala wa kizayuni wa Israel na Marekani kuishambulia Iran wakati wa vita vya kutwisha vya siku 12 dhidi ya Iran.
Kuhusiana na hili, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alidai Jumatano ya Julai 9 katika juhudi za wazi, ndani ya fremu ya vita vya kisaikolojia dhidi ya Iran na kuzusha hofu na wahka miongoni mwa raia wa Marekani kwamba: "Iran inataka kuwa na makombora ya masafa marefu yenye vichwa vya nyuklia ili kuwatishia."
Netanyahu, akihalalisha mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, alidai: "Kwa kuishambulia Iran, mimi na Trump tuliilinda na kuiepusha Marekani kutokana na hatari."
Marekani, pamoja na Israel, kwa miaka mingi zimekuwa zikiishutumu Iran kwamba, ina mpango wa kijeshi wa nyuklia, licha ya kutotoa ushahidi wowote, na imetekeleza hatua nyingi za kisiasa na vikwazo dhidi ya Iran kwa kisingizio hiki.
Kwa miaka mingi, nchi za Magharibi zimeishutumu Iran kwamba ina mpango wa kijeshi wa nyuklia, licha ya kutotoa ushahidi wowote, na zimetumia hili kama kisingizio cha kuchukua hatua kubwa za kisiasa na vikwazo dhidi ya Iran. Shutuma hizi zinatolewa huku Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikisema mara kwa mara kwamba sio tu kwamba haina mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia, bali hata haielekei upande huo.