Mazungumzo ya 'dhati' ya Iran na nchi tatu za Ulaya yafanyika Istanbul
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128772-mazungumzo_ya_'dhati'_ya_iran_na_nchi_tatu_za_ulaya_yafanyika_istanbul
Iran na nchi tatu za Ulaya ambazo ni Ufaransa, Uingereza na Ujerumani (zinazojulikana kama E3), wamekubaliana kuendelea na mashauriano kuhusu suala la vikwazo na mpango wa nyuklia wa Iran. Hayo ni kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi.
(last modified 2025-07-26T04:36:22+00:00 )
Jul 26, 2025 04:36 UTC
  • Mazungumzo ya 'dhati' ya Iran na nchi tatu za Ulaya yafanyika Istanbul

Iran na nchi tatu za Ulaya ambazo ni Ufaransa, Uingereza na Ujerumani (zinazojulikana kama E3), wamekubaliana kuendelea na mashauriano kuhusu suala la vikwazo na mpango wa nyuklia wa Iran. Hayo ni kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi.

Gharibabadi alitoa taarifa hiyo kupitia chapisho kwenye ukurasa wake wa X baada ya ya mazungumzo ya faragha yaliyofanyika katika ubalozi mdogo wa Iran jijini Istanbul, Uturuki.

Kikao hicho kilichodumu zaidi ya saa tatu siku ya Ijumaa, kilihudhuriwa na manaibu mawaziri wa mambo ya nje wa Iran, Majid Takht-Ravanchi na Gharibabadi, pamoja na wajumbe waandamizi kutoka nchi za E3. Mazungumzo haya yalifuatia duru kama hiyo iliyofanyika Mei 16 pia mjini Istanbul.

Katika chapisho lake, Gharibabadi amesema wajumbe wa Iran walifanya “mazungumzo ya kina, ya dhati na ya wazi” na Wazungu kuhusu “mwelekeo wa sasa kuhusiana na kuondolewa kwa vikwazo na masuala ya nyuklia.”

Ameongeza kuwa ujumbe wa Iran ulikosoa vikali misimamo ya E3 kuhusiana na “vita vya kijeshi vya kichokozi vinavyoendeshwa na Israel na Marekani dhidi ya watu wa Iran.”

Gharibabadi amesema: “Tulieleza misimamo yetu ya msingi, ikiwemo kuhusu kile kinachoitwa ‘snapback mechanism’", akimaanisha mpango wa kurejesha vikwazo kwa kasi dhidi ya Iran iwapo itaonekana kukiuka makubaliano ya nyuklia.

Amesema kuwa pande zote mbili ziliwasilisha mapendekezo maalum na kuchambua kwa undani vipengele mbalimbali vinavyohusiana navyo.

Katika mazungumzo ya wiki iliyopita na mawaziri wenzake wa Ujerumani, Ufaransa na Uingereza pamoja na Mkuu wa Sera za Kigeni wa EU, Kaja Kallas, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alisisitiza kuwa Umoja wa Ulaya na E3 lazima waachane na “sera za vitisho zilizochoka” iwapo wanataka kuwa na nafasi yoyote katika duru mpya ya mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na Marekani.

Akinukuu vitisho vya mara kwa mara vya Ulaya kuhusu kuanzishwa upya vikwazo kwa kutumia kipengele cha ‘snapback,’ Araghchi amesema, “Iwapo EU/E3 wanataka kushiriki kwa dhati, wanapaswa kuwa na uwajibikaji wa kweli, waachane na sera za vitisho zilizopitwa na wakati, zikiwemo zile za 'snapback' ambazo hawana msingi wowote wa kimaadili wala kisheria kuziendeleza.”