Kamanda: Majeshi ya Iran yako tayari kikamilifu kukabiliana na vitisho
Kamanda mkuu wa kijeshi wa Iran amesisitiza kuwa Majeshi ya Iran yako katika hali ya tahadhari kamili ili kukabiliana na vitisho vyovyote vya uvamizi kutoka kwa maadui wa nchi hii.
“Vikosi vya Majeshi viko tayari kikamilifu, vikiwa vinafuatilia kwa karibu harakati zozote za adui, ikiwa watafanya kosa la kimahesabu na kujaribu tena kuvamia ardhi takatifu ya nchi yetu, watapokea jibu kali zaidi,” amesema kamanda wa Kituo cha Kijeshi cha Khatam al-Anbiya siku ya Jumatano.
Kauli hii inakuja huku Jeshi la Majini la Iran likiwa limepanga kuanza awamu ya operesheni ya mazoezi ya makombora ya Eqtedar 1404 leo Alhamisi.
Msemaji wa Jeshi la Majini, Admeri Abbas Hassani, amesema mazoezi hayo ya siku mbili ya makombora yatafanyika katika Bahari ya Oman na Bahari ya Hindi Kaskazini.
Pia siku ya Jumatano, Waziri wa Ulinzi wa Iran, Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh, alisema makombora yaliyotumika na Majeshi ya Iran dhidi ya Israel katika vita vya siku 12 vya Juni yalitengenezwa nchini miaka michache iliyopita, akionya kwamba makombora mapya yenye uwezo bora zaidi yatatumika iwapo utawala wa Kizayuni wa Israel utatekeleza mashambulizi mengine.
Amesisitiza kuwa Majeshi ya Iran hayategemei zana za kigeni na kwani viwanda vya ulinzi vya Iran vinaunda zana za kutosha za kivita. Jenerali Nasirzadeh amesema dunia imeona kuwa makombora yaliyorushwa na Iran yalilenga malengo yake kwa usahihi na kusababisha uharibifu mkubwa kwa utawala wa Kizayuni.
Mnamo Juni 13, 2025, utawala wa Kizayuni ulianzisha uchokozi dhidi ya Iran, ukilenga taasisi kadhaa za kiraia, kijeshi, na nyuklia, jambo lililosababisha mauaji ya baadhi ya makamanda wa kijeshi wa Iran na wanasayansi wa nyuklia.
Katika kulipiza kisasi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilivurumisha makombora yaliyolenga ngome za utawala wa Kizayuni wa Israel katika operesheni iliyopewa jina la Ahadi ya Kweli III, ikisababisha uharibifu mkubwa katika makazi na vituo vya kijeshi.
Mnamo Juni 22, 2025, Jeshi la Anga na Majini la Marekani liliingia vitani na kutekeleza mashambulio ya anga dhidi ya vituo vitatu vya nyuklia vya Iran katika jaribio la kuusaidia utawala haramu wa Israel.
Siku iliyofuata, Juni 23, vikosi vya Iran vililipiza kisasi kwa kuvurumisha makombora 30 dhidi ya kambi ya jeshi la Marekani nchini Qatar na kusababisha hasara kubwa.
Hatimaye, Juni 24, baada ya mapigo makubwa kutoka Iran, utawala wa Kizayuni wa Isarel na Marekani walilazimika kukubali kusitisha mapigano.