Iran yalaani uchokozi wa mara kwa mara wa Israel dhidi ya Syria
-
Amir Saeid Iravani
Iran imelaani vikali vitendo vya uchokozi vya mara kwa mara vya Israel dhidi ya raia na miundombinu muhimu nchini Syria, na kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutopuuza hatua za utawala huo zinazovuruga amani.
Balozi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Amir Saeid Iravani, ameyasema hayo akihutubia kikao cha Baraza la Usalama kuhusu Syria jana Alhamisi.
Iravani amesema Iran inapinga kabisa jaribio lolote la kudhoofisha mamlaka ya Syria, kubadilisha muundo wake wa idadi ya watu, na kugawanya ardhi yake.
Alisema kuwa "Baraza la Usalama halipaswi kupuuza vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyoendelea kufanywa na utawala wa Israel nchini Syria."
"Mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel yamesababisha vifo vya raia, kuharibu miundombinu muhimu na kuzidisha mivutano ya kikanda," amesema.
Iravani ametoa wito wa kukomeshwa mara moja hatua ya Israel kukalia kwa mabavu eneo la Golan huko Syria, akitaja kitendo hicho kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa, Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na maazimio ya Baraza la Usalama.
Vilevile ameonya juu ya kuendelea kwa ugaidi nchini Syria akisema: Makundi ya Da'esh na Al-Qaida yanaendelea kuyumbisha Syria na kanda nzima, na kudhoofisha sana amani na usalama wa kikanda na kimataifa.
Vikosi vya jeshi la Israel vimejizatiti katika angalau maeneo tisa ndani ya kusini mwa Syria.