Larijani: Wamagharibi watambue kuwa Iran haiogopi vita
Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Iran, Ali Larijani, amethibitisha tena dhamira ya Tehran kushiriki katika mazungumzo ya kidiplomasia huku akionya kwamba mazungumzo ya maana yanaweza kusonga mbele tu endapo Marekani na Ulaya zitakubali kuwa mashinikizo na vitisho vya vita haviwezi kuwatisha wananchi wa Iran.
Katika mahojiano ya hivi karibuni na tovuti ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, Larijani amesisitiza kuwa diplomasia inaendelea kuwa nyenzo kuu ya Jamhuri ya Kiislamu, lakini ni pale tu inapofanyika kwa nia njema.
Ameongeza kuwa: “Ushauri wangu siku zote umekuwa kwamba Iran kamwe isiachane na diplomasia, kwa sababu diplomasia yenyewe ni chombo."
Aidha amesema: “Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesisitiza kwamba bendera ya mazungumzo lazima ibaki mikononi mwetu. Msimamo huu ni sahihi kabisa.”
Hata hivyo, Larijani ameonya kuwa mazungumzo hayawezi kufanikiwa iwapo madola ya Magharibi yatayachukulia kama kisingizio cha vitendo vya uhasama.
Amebainisha kuwa kauli za Magharibi kuhusu kuilazimisha Iran isalimu amri tayari zimeonesha kuwa hazina mashiko. “Katika vita hivi, wao wenyewe waligundua kuwa Wairani si watu wa kusalimu amri,” ameongeza.
Iran imepoteza imani zaidi na Marekani na washirika wake katika wiki za hivi karibuni. Mnamo Juni 13, utawala wa Kizayuni wa Israel ulitekeleza shambulio la kichokozi dhidi ya Iran, na kuua makamanda waandamizi wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia pamoja na raia.
Chini ya siku kumi baadaye, Marekani iliingia rasmi vitani kwa kushambulia kwa mabomu vituo vitatu vya nyuklia vya amani, ambavyo vilikuwa chini ya ukaguzi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), hatua iliyokiuka Mkataba wa Umoja wa Mataifa na Mkataba wa Kuzuia Kuenea Silaha za Nyuklia (NPT).
Mashambulizi haya yalitokea wakati ambapo Iran na Marekani, kwa upatanishi wa Oman, zilikuwa zimefanya duru tano za mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja tangu mwezi Aprili na zilikuwa zinajiandaa kwa duru mpya ya mazungumzo mjini Muscat mnamo Juni 15.
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa Iran kujiondoa kwenye Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia (NPT) iwapo mashinikizo dhidi yake yataongezeka, Larijani amesema uwezekano huo umekuwepo daima.
Larijani pia amekosoa juhudi za Ulaya za kufufua kile kinachoitwa “mfumo wa kurejesha vikwazo (snapback mechanism),” na kusema hatua hiyo itadhoofisha ushirikiano.
Ameongeza kuwa mataifa ya Ulaya kimsingi yanatekeleza ajenda ya Marekani.”
Mfumo wa snapback unalenga kufufua maazimio sita ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran.