Iran yasambaratisha mtandao wa magaidi waliokuwa na silaha za Marekani
Maafisa wa usalama nchini Iran wamefanikiwa kusambaratisha mtandao wa kigaidi katika mkoa wa Sistan na Baluchestan, kusini mashariki mwa nchi, karibu na mpaka wa Pakistan, na kuwaua magaidi sita huku wakikamata wawili.
Idara ya Usalama ya Mkoa wa Sistan na Baluchestan imesema katika taarifa yake kwamba kikundi hicho cha magaidi kimesambaratishwa katika operesheni kubwa ya kupambana na ugaidi, ambayo ilisababisha kunaswa kwa silaha mbalimbali, risasi, na vifaa vya mlipuko.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa magaidi hao, ambao walikuwa wamevuka mpaka wa mashariki katika siku za karibuni, walikamatwa baada ya kutambuliwa na vikosi vya usalama. Walikamatwa kabla ya kutekeleza hujuma za kigaidi.
Kikundi hicho kilijumuisha wapiganaji saba wasiokuwa Wairani, wakiwa na silaha mbalimbali zikiwemo RPG zenye miongozo ya laser, bunduki za Kimarekani aina ya M4 na M16, mabomu ya mkono, vesti za za kusheheni mabomu na vifaa vya mawasiliano. Katika mapigano makali yaliyodumu kwa masaa kadhaa, magaidi sita waliuawa na wawili walikamatwa wakiwa hai.
Maafisa watatu wa usalama wa Iran wamejeruhiwa katika tukio hilo.
Idara ya Usalama ya Mkoa wa Sistan na Baluchestan imesema kwamba magaidi hao walikuwa wanapanga shambulizi dhidi ya "kituo muhimu" mashariki mwa Iran
Mbinu walizokuwa wanatumia magaidi hao zinakaribiana sana na mbinu zinazotumiwa na shirika la ujasusi la Israel, Mossad.
Mkoa wa Sistan na Baluchestan, unaopakana na Pakistan, umeathiriwa na mashambulizi kadhaa ya kigaidi dhidi ya raia na vikosi vya usalama katika miaka ya hivi karibuni.
Makundi ya kigaidi yanayoshambulia maslahi ya Iran katika maeneo ya kusini mashariki na kusini magharibi ya nchi yanadhaniwa kuwa na uhusiano na mashirika ya kijasusu ya kigeni.
Mnamo Oktoba 26 mwaka jana, maafisa kumi wa vikosi vya usalama vya Iran waliuawa katika shambulizi la kigaidi katika wilaya ya Gohar Kuh, kaunti ya Taftan.
Kikundi cha kigaidi kinachojiita Jaish al-Adl kulikiri kuhusika na shambulizi hilo.