Zarif aipongeza Lebanon kwa kuipigisha magoti Israel
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemuandikia barua mwenzake wa Lebanon kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 10 ya ushindi wa nchi hiyo dhidi ya askari vamizi wa utawala haramu wa Israel.
Kwenye barua hiyo kwa Gebran Bassil, Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon, Muhammad Javad Zarif amesema ushindi huo dhidi ya Wazayuni maghasibu ulipatikana kutokana na kujitolea muhanga wanamuqawama wa Hizbullah kwa shabaha ya kupatikana uhuru, haki na historia yenye izza kwa taifa la Lebanon na mataifa mengine katika eneo hili.
Muhammad Javad Zarif kadhalika amemuandikia barua Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon na kubainisha kuwa, ushindi huo katika vita vya siku 33 mnamo Julai mwaka 2006, kati ya Lebanon na wanajeshi wa utawala haramu wa Israel sio tu fahari kwa Lebanon, bali kwa ulimwengu wa Kiislamu na mataifa yanayopenda haki, uhuru wa kujitawala na uhuru wa kulinda ardhi zao.
Haya yanajiri siku chache baada ya Ali Larijani, Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani bunge la Iran kumtumia ujumbe wa fanaka Sayyid Nasrullah kwa mnasaba wa maadhimisho hayo. Katika ujumbe wake huo, Dakta Larijani alisema kuwa, hivi karibuni ulimwengu utashuhudia ushindi wa mwisho wa kambi ya muqawama na mapambano dhidi ya magaidi wa kitakfiri na waungaji mkono wao katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kwa ujumla.
Akizungumza Ijumaa iliyopita kwa mnasaba wa maadhimisho hayo mjini Beirut, Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon aliyataka makundi ya kigaidi na kitakfiri kuweka chini silaha na yatambue kuwa harakati zao hazina maslahi kwa yeyote isipokuwa adui Marekani.