Kiongozi Muadhamu awataka Wairani wote kushiki kwenye zoezi la uchaguzi ujao
(last modified Wed, 24 Feb 2016 15:52:09 GMT )
Feb 24, 2016 15:52 UTC
  • Kiongozi Muadhamu awataka Wairani wote kushiki kwenye zoezi la uchaguzi ujao

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza udharura wa wananchi wote wa Iran kushiriki katika uchaguzi wa Bunge la Baraza la Watalamu kwa shabaha ya kuzima na kubatilisha njama za maadui.

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo akihutubia hadhara kubwa ya wananchi wa Najafabad. Ameashiria chaguzi mbili muhimu sana za Bunge na Baraza la Watalamu zitakazofanyika siku ya Ijumaa na kusema: Umuhimu wa uchaguzi nchini si kupiga kura pekee bali uchaguzi una maana ya kutunisha kifua na misuli kwa taifa la Iran mbele ya adui baada ya aina mbalimbali za mashinikizo, vikwazo vya kidhalimu na propaganda chafu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Ametoa maelezo ya kina kuhusu msamiati wa "misimamo ya kati na misimamo mikalia" na kutoa wito kwa wananchi wote hususan viongozi na wanasiasa kuwa macho mbele ya njama za adui za kutaka kuzusha kambi mbili bandia na za kutwisha katika nga ya sasa ya uchaguzi. Amesema kuwa uchaguzi ujao ni medani ya kutunisha kifua kitaifa, kuonesha uaminifu, kusimama kidete kwa taifa na kulinda heshima na kujitawala. Amesisitiza kuwa, watu wote wanaoitakia izza na heshima Iran ya Kiislamu wanapaswa kushiriki katika uchaguzi wa Ijumaa ijayo hapa nchini na kwamba tarehe 7 Esfand (26 Februari) dunia itaona jinsi wananchi wa Iran watakavyohudhuria kwa wingi na kwa hamu kubwa kwenye masanduku ya kupigia kura.

Ayatullah Khamenei amesema taifa la Iran linataka bunge linaloshikamana na dini, lenye kuwajibika, shujaa, lisilohadaika, ngangari katika kukabiliana na tamaa na tabia ya kutaka kujitanua ya ubeberu, linalolinda heshima na kujitawala kwa taifa, linalotaka maendeleo halisi ya nchi, lenye imani na harakati ya kielimu ya vipawa vya vijana, lenye imani na uchumi unaotegemea uzalishaji wa ndani ya nchi, linalojua vyema mashaka na matatizo ya wananchi, lenye azma ya kutatua matatizo hayo, lisilotishika mbele ya Marekani na linalotekeleza vyema majukumu yake ya kisheria.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia mipango ya Marekani kwa ajili ya kipindi cha baada ya kufikiwa mapatano ya nyuklia (kati ya Iran na kundi la 5+1) na kusema: Baada ya makubaliano hayo Wamarekani walikuwa na mpango kwa ajili ya Iran na mpango mwingine kwa ajili ya eneo la Mashariki ya Kati na wangali wanafuatilia mipango hiyo kwa sababu wanajua vyema ni nchi gani inayosimama imara kukabiliana na malengo yao machafu katika eneo hili. Ayatullah Khamenei amesema Wamarekani wanatumia vibaraka katika kutekeleza mipango yao nchini Iran. Vilevile amewataka wanasiasa kutyokariri misamiati ya kisiasa inayotumiwa na adui hususan utumiaji wa maneno ya misimamo mikali na misimamo ya wastani.

Tags