Iran yaitaka EU kuacha kulikingia kifua kundi la kigaidi la MKO
Katibu wa Tume ya Haki za Binadanamu ya Idara ya Mahakama za Iran amemwandikia barua Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya akitaka kuondolewa kinga kwa kundi la kigaidi la Munafiqiin (MKO) katika nchi za Magharibi.
Katika barua hiyo Dakta Muhammad Javad Larijani amemwambia Bi Federica Mogherini kwamba, ulipuaji wa mabomu katika mikusanyiko na mikutano ya raia ni kielelezo cha wazi zaidi cha ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na kundi la kigaidi la MKO nchini Iran.
Dakta Larijani ameashiria jinai na mauaji yaliyofanywa na kundi hilo la kigaidi la Munafiqii dhidi ya taifa la Iran na kusema: Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapo mwaka 1979, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa miongoni mwa wahanga wakubwa zaidi wa ugaidi na katika kipindi hicho maelfu ya wanadamu wasio na hatia yoyote wameuawa na wengine kujeruhiwa.
Katibu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Idara ya Mahakama hapa nchini amesema kuwa, kundi la kigaidi la Munafiqiin mbali na kutenda jinai za kutisha dhidi ya taifa la Iran, tangu mwaka 2011 limekuwa likishirikiana na magaidi katika nchi za Syria na Iraq na kuua watu wengi katika nchi hizo. Amesema inasikitisha kuona kwamba, wanachama wa kundi hilo la kigaidi wanatembea kwa uhuru kamili na bila ya kufuatiliwa katika nchi za Ulaya na baadhi yao wamezifanya nchi hizo kuwa maficho salama.

Dakta Muhammad Javad Larijani amesema kuwa, baadhi ya nchi zinazodai kutetea haki za binadamu zinalitambua kundi hilo la kigaidi kuwa linatetea na kulinda haki za binadamu licha ya mikono ya wanachama wake kuchafuka kwa damu za maelfu ya wanawake na watoto wadogo wasio na hatia. Amesisitiza kuwa, mapambano dhidi ya hatari ya ugaidi na mgogoro wa wakimbizi yanahitaji azma kubwa na ya kweli na kusema: Siasa za kindumakuwili kuhusu suala la haki za binadamu na kuyaunga mkono makundi ya kigaidi ambayo mikono ya wanachama wao imejaa damu ya maelfu ya Wairani hakuwezi kutetewa kwa njia yoyote ile.
Dakta Larijani ametoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuwakamata na kuwafungulia mashtaka viongozi na wanachama waliotenda jinai wa kundi hilo huko barani Ulaya.