Iran yamuangamiza mmoja wa vinara wa ISIS mpakani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i20401-iran_yamuangamiza_mmoja_wa_vinara_wa_isis_mpakani
Vikosi vya usalama vya Iran vimefanikiwa kumuangamiza mmoja kati ya vinara wa kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) katika eneo la mpakani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 29, 2016 03:47 UTC
  • Waziri wa Usalama wa Iran, Sayyed Mahmoud Alawi
    Waziri wa Usalama wa Iran, Sayyed Mahmoud Alawi

Vikosi vya usalama vya Iran vimefanikiwa kumuangamiza mmoja kati ya vinara wa kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) katika eneo la mpakani.

Akizungumza Jumatatu usiku, Waziri wa Usalama wa Iran Sayyed  Mahmoud Alawi amesema, kinara huyo wa magaidi wa ISIS aliyekuwa akijulikana kama Abu Aisha Kurdi ametambuliwa na kuangamizwa na maafisa hodari wa usalama nchini.

Sayyed Mahmoud Alawi ameongeza kuwa, vikosi vya usalama vya Iran katu havitamruhusu adui adhuru usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Akizungumza katika hafla ya maombolezo ya kuaga dunia Mtume Muhammad SAW na kuuawa Shahidi Imam Hassan Mujtaba AS katika mji wa Karaj magharibi mwa Tehran, Waziri wa Usalama Iran ameongeza kuwa, umoja wa taifa la Iran ni sababu muhimu ya kuangamizwa njama za maadui wa nchi hii.

Kinara wa ISIS, Abu Aisha Kurdi aliyeagamizwa na vikosi vya usalama vya Iran

Ameongeza kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yana maadui wengi sana lakini umoja baina ya wananchi na mihimili ya dola ni sababu ya taifa hili kuibuka mshindi mbele ya njama za maadui na kusambaratisha njama dhidi yake.

Sayyed Mahmoud Alawi aidha ameashiria ulazima wa kuhimiza maadili mema katika jamii na kuongeza kuwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalianzishwa kwa lengo la kueneza utamaduni  na mafundisho ya Mtume SAW katika jamii.

Magaidi wanaopata uungaji mkono wa madola ya kigeni wamekuwa wakifanya njama za mara kwa mara za kujipenyeza kwenye mipaka ya Iran ili kueneza ukatili wao, hata hivyo njama zao zimekuwa zikishindwa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa macho askari wa kulinda usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa ushirikiano kamili wa wananchi.