'Iran itatoa jibu kali baada ya Marekani kukiuka mapatano ya nyuklia'
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i20620-'iran_itatoa_jibu_kali_baada_ya_marekani_kukiuka_mapatano_ya_nyuklia'
Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran amesema hatua ya Bunge la Congress la Marekani kurefusha vikwazo dhidi ya Iran ni ukiukaji wa wazi wa mapatano ya nyuklia baina ya Iran na madola sita makubwa duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 02, 2016 12:43 UTC
  • 'Iran itatoa jibu kali baada ya Marekani kukiuka mapatano ya nyuklia'

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran amesema hatua ya Bunge la Congress la Marekani kurefusha vikwazo dhidi ya Iran ni ukiukaji wa wazi wa mapatano ya nyuklia baina ya Iran na madola sita makubwa duniani.

Ayatullah Mohammad Ali Muwahidi Kermani, khatibu na imamu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran wiki hii amesema, kupitishwa muswada wa vikwazo vya miaka 10 dhidi ya Iran (D'Amato) katika mabaraza ya wawakilishi na senate nchini Marekani ni ukiukwaji wa wazi wa mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Aidha amesema Iran itatoa jibu kali kwa hatua hiyo ya Marekani.

Ayatullah Kermani amesema kupitishwa muswada huo ni ishara ya wazi kuwa, kukiuka mapatano, kutoaminika, ukhabithi na kuvunja ahadi ni dhati ya Marekani.

Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran ameongeza kuwa, hakuna tarajio lololote kutoka kwa Marekani isipokuwa uadui na kwamba,  daima Iran imekuwa na dhana mbaya kwa Marekani kutokana na historia yake ya kuvunja ahadi na kuhadaa.

Sala ya Ijumaa Tehran

Ikumbukwe kuwa, Januari mwaka huu, Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambazo ni Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Marekani pamoja na Ujerumaini, zilianza kutekeleza makubaliano hayo ya nyuklia ambayo yalitiwa saini tarehe 14 Julai, 2015 mjini Vienna nchini Austria.

Akiendelea na hotuba yake, Ayatullah Kermani amesema jinai ya Saudia dhidi ya Mahujaji huko Mina katu haitosahaulika na kuongeza kuwa, jinai hiyo na jinai nyinginezo za Saudia zinapaswa kutajwa mara kwa mara ili Waislamu wafahamu kuwa ukoo wa Aal Saudi haustahiki wala hauwezi kusimamia ibada ya Hija.

Ayatullah Kermani pia ameashiria mafanikio ya majeshi ya Iraq na Syria na vikosi vya kujitolea vya wananchi katika nchi hizo katika kukabiliana na kundi la kigaidi la ISIS au Daesh na kusema, mafanikio haya yatawaokoa wananchi wasio na hatia na dhulma na ukatili wa kundi hilo la kigaidi.

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran pia amepongeza Jeshi la Majini la Iran kwa uwepo wake katika maji ya kimataifa na kusema hilo linafanyika kwa ajili ya kuleta amani na utulivu.