Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu kujitolea mashahidi
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja mawimbi ya njama na mashambulizi ya uistikbari katika kadhia mbalimbali duniani kuwa yalikuwa ni kwa ajili ya Iran ya Kiislamu na kueleza kuwa, kutawala Qur'ani na dini nchini Iran na kueneza masuala hayo katika pembe nyingine za dunia, ni sababu iliyomfanya adui ahisi hatari na hivyo kufanya njama na kuendesha harakati dhidi ya mfumo wa Kiislamu wa Iran.
Akizungumza na wawakilishi wa taasisi inayoandaa marasimu ya kuwakumbuka mashahidi elfu nne wa mkoa wa Golestan ambayo yalifanyika tarehe 5 mwezi huu wa Disemba, na matini ya ujumbe wake kusomwa leo katika eneo palipofanyika kumbukumbu hiyo huko Gorgan, Ayatullah Khamenei amekutaja kujitolea mashahidi katika kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu, heshima ya taifa, mustakbali na historia ya Iran kuwa ni tukio adhimu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, iwapo kusingekuwepo kujitolea huko na watu hawa wangekuwa wasiopenda kuuawa shahidi mbegu changa za Mfumo wa Kiislamu zisingeweza kukabiliana na vimbunga vigumu, na hatimaye ungesambaratika; kwa msingi huo moyo wa kujitolea unapaswa kulindwa na kuimarishwa. Marasimu ya kuwakumbuka mashahidi elfu nne wa mkoa wa Golestan yalianza shughuli zake leo asubuhi katika mji wa Gorgan kwa hotuba ya Ali Larijani Spika wa Majlisi ya Kiislamu ya Iran (bunge).