Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran aonya kuhusu jinai za Saudia, Bahrain
Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran ameonya kuhusu mauaji na ukandamizaji unaofanywa na tawala za kikoo za Saudi Arabia na Bahrain dhidi ya mataifa ya Waislamu na kusema tawala hizo zinaelekea kusambaratika kutokana na jinai zao hizo.
Katika hotuba za Swala ya Ijumaa wiki hii mjini Tehran, Ayatullah Muhammad Muwahhidi Kermani ameashiria migogoro ya sasa katika nchi za Bahrain, Yemen na Syria na kusema chanzo cha migogoro hiyo ni ukatili wa tawala za Aal Saud na Aal Khalifa na mamluki wao.
Imamu wa muda wa Swala ya Ijumaa Tehran pia ameipongeza Syria na harakati ya mapambano kwa ushindi mkubwa dhidi ya magaidi huko Aleppo na kusema: "Kutimuliwa magaidi huko Aleppo si tu kuwa ni ushindi wa kijeshi bali ni ushindi wa haki mbele ya batili na ni kashfa kubwa kwa tawala za Magharibi na za Kiarabu zinazowaunga mkono magaidi."
Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran pia ameashiria hamasa ya Tisa Dey nchini Iran na kusema siku hii ilikuwa siku ya wananchi kumbai Kiongozi Muadhamu, siku ya mwamko na umoja wa kitaifa nchini Iran na kushindwa njama za madola ya kibeberu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ayatullah Kermani amegusia hatua ya Marekani kukiuka mapatano yake ya nyuklia na Iran na kusema leo imewabainikia watu wote kuwa Marekani ni adui wa taifa la Iran na hivyo haipaswi kuamini ahadi za uongozi za nchi hiyo.