Ayatullah Siddiqi: Utawala wa kifalme Bahrain umepoteza uhalali wake
Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuwa, kunyongwa vijana watatu Waislamu wa Kishia nchini Bahrain kumeufanya utawala wa kifalme wa nchi hiyo wa Aal Khalifa upoteze uhalali wake.
Hujjatul Islam Walmuslimiin Sheikh Kazem Seddiqi amesema hayo mbele ya hadhara ya maelfu ya waumini waliohudhuria ibada ya Sala ya Ijumaa mjini Tehran na kuongeza kuwa, wananchi wa Bahrain wamekuwa wakipigania uhuru na haki zao za kimsingi lakini utawala wa kifamilia wa nchi hiyo badala ya kusikiliza kilio na matakwa ya wananchi umeendelea kutumia mkono wa chuma kukandamiza harakati za wananchi hao.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amekosoa vikali siasa za utawala wa Aal Khalifa na kueleza kuwa, hivi sasa magereza na jela za nchi hiyo zimejaa maulamaa na wapigania uhuru wa nchi hiyo.
Ayatullah Kazem Seddiqi aidha ameashiria mkutano wa tarehe 23 na 24 za mwezi huu wa Januari huko Astana Kazakhstan kuhusu mgogoro wa Syria na kusema kuwa, ana matumaini mkutano huo utapelekea kuokolewa raia wa vijiji viwili ya Syria ambao wamo katika mzingiro wa makundi ya kigaidi.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amezungumzia kukaribia maadhimisho ya Alfajiri Kumi na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na kubainisha kwamba, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ulikuwa mlipuko wa nuru, muujiza wa Ulimwengu wa Kiislamu na dhihirisho la nguvu, imani na umaanawi wa wananchi wa Iran; mapinduzi ambayo yaliteteresha nguzo na misingi ya madola makubwa ya Mashariki na Magharibi.