Iran yawakamata magaidi wa ISIS karibu na Tehran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i25001-iran_yawakamata_magaidi_wa_isis_karibu_na_tehran
Iran imewakamata wafuasi wa kundi kigaidi la ISIS au Daesh katika viunga vya mji mkuu Tehran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 11, 2017 10:36 UTC
  • Iran yawakamata magaidi wa ISIS karibu na Tehran

Iran imewakamata wafuasi wa kundi kigaidi la ISIS au Daesh katika viunga vya mji mkuu Tehran.

Katika taarifa, Mwandesha Mashtaka Mkuu wa Iran Ja'afar Montazeri amesema wafuasi hao wa kundi la kigaidi na kitakfiri la ISIS walikuwa wanapanga njama ya kutekeleza hujuma mjini Tehran jana Ijumaa wakati wa sherehe za kuadhimisha mwaka wa 38 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Mamillioni ya Wairani walijitokeza mitaani katika matembezi hayo ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979 ambapo nchi hii  iliyokuwa chini ya utawala wa kiimla wa Shah ambaye alikuwa kibaraka wa Marekani.

Mwandesha Mashtaka Mkuu Ja'afar amesema kwa kuzingatia kuwa Iran inahusika na vita dhidi ya ugaidi nje ya mipaka yake hasa Syria na Iraq, kundi la ISIS lilikuwa linapanga kutekeleza oparesheni za kigaidi hapa nchini.  Amesema taarifa zaidi kuhusu njama za magaidi hao wa ISIS zitatangazwa kwa umma katika kipindi cha siku chache zijazo.

Afisa huyo wa ngazi za juu katika vyombo vya mahakama Iran amesisitiza kuwa, iwapo Iran haingeunka mkono mikakati ya kupambana na magaidi, leo hii magaidi wa ISIS wangekuwa wanazunguka bila wasi wasi ndani ya nchi hii. Amesema iwapo Iran haitokabiliana na maadui nje ya mipaka yake, basi wataingia nchini bila kizuizi.

Matembezi ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Iran imekuwa ikitoa ushauri wa kijeshi kwa Syria na Iraq kufuatia maombi ya nchi hizo mbili ambazo ziko mstari wa mbele katika vita dhidi ya magaidi hasa wa ISIS.

Mwezi Agosti mwaka 2016 maafisa wa usalama Iran walimuua afisa mwenye ushawishi katika kundi la magaidi wakufurishaji wa ISIS na kusambaratisha mtandao wa kigaidi magharibi mwa nchi.

Katika miezi ya hivi karibuni maafisa wa usalama wa Iran wamepambana na magaidi na kuzuia njama zao za kujipenyeza na kutekeleza hujuma nchini huku idadi kubwa ya silaha zikikamatwa mikononi mwa magaidi hao.