Mar 01, 2017 15:34 UTC
  • Marais Rouhani na Erdogan wazungumzia uhusiano wa Iran na Uturuki

Marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki wamekutana na kufanya mazungumzo kuhusu masuala mbali mbali likiwemo la umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

Rais Hassan Rouhani wa Iran na mwenzake wa Uturuki, Racep Teyyip Erdogan wamefanya mazunguzo hayo pambizoni mwa kikao cha 13 cha viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ECO huko mjini Islamabad Pakistan na pia wamejadili suala la kupambana na ugaidi.

Mbali na masuala ya ugaidi na kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika nyuga tofauti, wawili hao pia wamezungumzia masuala ya kieneo na kimataifa.

Marais wa Iran na Uturuki wakiongea pambizoni mwa kikao cha ECO, Pakistan

Marais wa Iran na Uturuki wamesisitizia umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa pande mbili wa Tehran na Ankara haswa kwa kutilia maanani kuwa nchi mbili hizi ni majirani.

Wakati huo huo, Mevlut Cavusoglu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ameliambia shirika la habari la IRNA kuwa, serikali ya Ankara inaishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kusimama na taifa hilo katika jaribio lililofeli la mapinduzi Julai 15 mwaka uliopita 2016.

Awali akihutubu katika mkutano huo wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ECO, Rais Hassan Rouhani wa Iran alisema mataifa yanayostawi kiuchumi barani Asia yataufanya uchumi wa dunia utoke Magharibi na kuelekea Mashariki na mabadiliko hayo yatapelekea bara hilo kuwa mbele karibuni hivi.

Dakta Rouhani amefafanua kuwa, roho ya uchumi wa dunia karibuni hivi itadundia barani Asia kuanzia nusu ya pili ya karne ya 21.

Marais wa Iran na Uturuki na jumbe zao huko Pakistan

 

Tags