Iran yawawekea vikwazo Wamarekani kujibu uchokozi wa dola hilo la kibeberu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i29250-iran_yawawekea_vikwazo_wamarekani_kujibu_uchokozi_wa_dola_hilo_la_kibeberu
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeongeza idadi ya watu na mashirika ya Marekani katika orodha ya vikwazo vyake ikiwa ni kujibu hatua kama hiyo iliyochukuliwa na Marekani dhidi ya Iran. 
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 18, 2017 09:52 UTC
  • Iran yawawekea vikwazo Wamarekani kujibu uchokozi wa dola hilo la kibeberu

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeongeza idadi ya watu na mashirika ya Marekani katika orodha ya vikwazo vyake ikiwa ni kujibu hatua kama hiyo iliyochukuliwa na Marekani dhidi ya Iran. 

Itakumbukwa kuwa jana Jumatano, Rais wa Marekani Donald Trump aliongeza idadi ya raia wa Iran na mashirika ya Kiirani na ya nje katika orodha ya waliowekewa vikwazo vya upande mmoja na Marekani kwa madai ya kuhusika katika mradi wa makombora wa Iran.

Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa tamko na kusema kuwa, mradi wake wa makombora utaendelea kwa nguvu zote kama ilivyopangwa na kamwe hautosita. 

Kijiji cha makombora cha chini ya ardhi nchini Iran

Tamko la wizara ya mambo ya nje ya Iran limetolewa leo ili kujibu hatua ya serikali ya Marekani ya kuongeza idadi ya watu na mashirika ya Iran na ya nje katika orodha ya vikwazo vyake dhidi ya Iran kutokana na mradi wake wa makombora. Iran imelaani kitendo hicho cha kichokozi cha Marekani na kusema ni kiyume cha sheria, hakikubaliki kabisa na kinakwenda kinyume na sheria za kimataifa.

Kwa mara nyingine, wizara ya mambo ya nje ya Iran imesisitiza kuwa ni haki ya Tehran ya kisheria na isiyokanushika, kuwa na uwezo wa kujilinda. Tamko la wizara hiyo limeongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea na mradi wake wa makombora kwa kuzingatia sheria za kimataifa na kwa ajili ya kulinda uhuru wake wa kisiasa na usalama wa Iran nzima.

Imesema, mradi wa makombora wa Iran hauendi kinyume na azimio nambari 2231 la Umoja wa Mataifa hivyo Tehran itaendelea nao kwa nguvu zote na kwa mujibu wa mipango iliyopo humu nchini.

 

Iran inaamini kuwa nguvu zake za kijeshi ni moja ya sababu zinazowafanya maadui waogope kuanzisha vita dhidi yake.