Iran: Hakuna kinachoweza kutuzuia tusijiimarishe kiulinzi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i30558-iran_hakuna_kinachoweza_kutuzuia_tusijiimarishe_kiulinzi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametetea msimamo wa nchi yake wa kutumia kikamilifu haki yake ya kujiimarisha kwa makombora na kusisitiza kuwa, hakuna kitu chochote kinachoweza kuizuia Tehran kutumia haki yake hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 16, 2017 12:52 UTC
  • Iran: Hakuna kinachoweza kutuzuia tusijiimarishe kiulinzi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametetea msimamo wa nchi yake wa kutumia kikamilifu haki yake ya kujiimarisha kwa makombora na kusisitiza kuwa, hakuna kitu chochote kinachoweza kuizuia Tehran kutumia haki yake hiyo.

Bahram Qassemi amesema hayo leo Ijumaa kujibu uamuzi wa Baraza la Sanate la Marekani wa kuiwekea vikwazo vipya Iran kutokana na mradi wake wa makombora. Qassemi amesema:

Mradi wa kujilinda kwa makombora wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unafanyika kwa mujibu wa sheria kikamilifu na wala haukinzani na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nambari 2231, hivyo hakuna yeyote awezaye kuizuia Tehran kuendelea na miradi yake ya ulinzi.

Moja ya makombora ya Iran

 

Jana Alkhamisi, Baraza la Sanate la Marekani lilipasisha kwa kura nyingi muswada wa kuiwekea vikwazo vipya Iran kutokana na mambo mbalimbali ikiwemo mradi wake wa makombora.

Muswada huo itabidi upasishwe pia na bunge la Congress la Marekani linaloongozwa na wabunge wa chama cha Republican cha rais wa nchi hiyo Donald Trump ambaye anatangaza wazi chuki zake dhidi ya Iran. Hatimaye utakuwa sheria kwa kutiwa saini na Trump.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amepinga vikali madai yanayotolewa na Marekani kuhusu mradi wake wa makombora na kusema kuwa kupasisha vikwazo vipya dhidi ya Tehran kutokana na mradi huo ni jambo lisilokubalika kabisa.

Vile vile amesema, uadui wa Marekani dhidi ya taifa la Iran ni mkubwa na ni wa muda mrefu na haishangazi kuona inatumia visingizio visivyoingia akilini kuiwekea vikwazo Iran.