Waziri wa Ulinzi wa Iran asema ISIS haina uhusiano wowote na Uislamu
Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema kundi la kigaidi la ISIS au Daesh halina uhusiano wowote na Uislamu na ni tishio kwa dunia nzima.
Brigedia Jenerali Hussein Dehqan ameyasema hayo Jumatano alipokuwa akizungumza na waandishi habari mjini Tehran na kuongeza kuwa, ISIS sasa ni aina fulani ya idiolojia ambayo haitumii mantiki hata kidogo na wala haina dini na hivyo kuna haja kwa dunia kuwa na irada na azma kubwa ya kukabiliana na fikra hiyo potovu.
Brigedia Jenerali Dehqan ameashiria kushindwa ISIS nchini Iraq na Syria na kusema: "Kundi la kigaidi la ISIS limepoteza vituo vyake vikuu na sasa limebakia tu katika muundo wa watu waliosambaratika ambao wanaweza kutenda vitendo hatari na hivyo kuna haja ya nchi zote kuchukua tahadhari.
Waziri wa Ulinzi wa Iran ameashiria matamshi ya kuingiliaji mambo ya nchi nyingine yaliyotolewa na Waziri wa Ulinzi wa Marekani kuhusu Iran na kusema: "Marekani imekuwa na tabia kama hizo katika kipindi cha miongo minne sasa na jambo hilo limeyafanya mataifa yote yaichukie Marekani na kupelekea nchi hiyo kudhoofika duniani. Brigedia Jenerali Dehqan amaesema watu wa Iran kwa mara kadhaa wamewafanya Wamarekani wajute kuhusu vitendo vyao vya uhasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Waziri wa Ulinzi wa Iran alikuwa akiashiria matamshi ya Wziri wa Ulinzi wa Marekani James Mattis ambayeo hivi karibuni alisema Marekani inapanga kuuangusha mfumo wa Kiislamu unaotawala nchini Iran.