Iran na Afrika Kusini zajadili namna ya kuimarisha uhusiano wao
Wanadiplomasia wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Afrika Kusini wamefanya mazungumzo hapa mjini Tehran kuhusu namna ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili hususan katika uga wa siasa.
Hussein Jaberi Ansari, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekuatana na mwenzake wa Afrika Kusini, Nomaindiya Mfeketo na kujadili masuala mbalimbali na kusisitiza haja ya kuimarishwa uhusiano wa Tehran na Pretoria katika nyuga za siasa, utamaduni na uchumi.
Masuala mengine ambayo yamejadiliwa na wanadiplomasia hao wa ngazi za juu wa Iran na Afrika Kusini ni kuunga mkono haki za Wapalestina, kupambana na ugaidi na misimamo mikali ya kufurutu ada na umuhimu wa kutumiwa njia za kidiplomasia na kisiasa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria.
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa, nchi hiyo ya Kiafrika inaunga mkono suala la kuasisiwa nchi huru ya Palestina ili kuhitimisha mzozo wa Mashariki ya Kati.
Kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika ni katika ajenda kuu ya sera za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Rais Hassan Rouhani ambaye alihifadhi kiti chake katika uchaguzi wa Mei mwaka huu amekuwa akisisitiza kuwa, Tehran itaendelea kuimarisha uhusiano wake na nchi za Afrika katika nyuga za uchumi, siasa na utamaduni.