Mtazamo maalumu wa Iran kuhusu bara la Afrika
Katika mazungumzo yake na Spika wa Bunge la Afrika Kusini, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inalipa umuhimu mkubwa suala la kuimarisha uhusiano wake na nchi zote za Afrika.
Rais Rouhani alisema hayo jana Jumamosi wakati alipoonana na Bi Baleka Mbete, Spika wa Bunge la Afrika Kusini hapa mjini Tehran. Ameongeza kuwa, Tehran iko tayari kuimarisha ushirikiano wake na Pretoria katika uga wa kiuchumi ikiwemo sekta za madini na nishati kama ambavyo iko tayari pia kuipa Afrika Kusini uzoefu wake wa kiufundi na kiteknolojia.
Kwa kuzingatia uhusiano mzuri wa kisiasa baina ya Iran na Afrika Kusini kutokana na nchi mbili kuwa na misimamo ya pamoja katika masuala mengi ya kieneo na kimataifa. Kiwango hicho ya ushirikiano wa kisiasa kinaweza kuwa msingi muhimu wa kuimarisha uhusiano wa Tehran na Pretoria katika nyuga nyinginezo hususan za kiuchumi. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Afrika Kusini kila moja ina suhula na nafasi nzuri ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kwa namna fulani kila upande unaweza kuudhaminia upande mwingine mahitaji yake na pia kupata masoko mapya.
Soko kubwa la Afrika ni eneo zuri la kuweza Iran kuuza bidhaa zake na pia kununua vitu inavyovihitajia. Ndio maana bara la Afrika likawa na nafasi muhimu katika siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Siasa za mambo ya nje za Iran zimesimama juu ya msingi wa kutoelekea upande mmoja tu, bali kuhakikisha inakuwa na uhusiano mzuri na mabara yote ya dunia likiwemo bara la Afrika. Kuhusiana na jambo hilo, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Kufungua mwavuli wa kidiplomasia kwa ulimwengu mzima na kutongángánia kuwa na uhusiano na baadhi ya nchi tu, ni mambo ambayo yanapaswa yapewe mazingatio maalumu katika siasa za nje za Iran.
Kwa kuzingatia nukta hiyo muhimu na ya kimsingi, bara la Afrika lina nafasi na fursa nyingi za kiuchumi kwa ajili ya Jamhuri ya Kislamu ya Iran na ni fursa nzuri pia kwa Iran ya kutumia udiplomasia amilifu kufanya harakati nyingi katika soko lenye ushindani mkubwa la bara la Afrika. Kiujumla ni kwamba, Iran ina nia ya kweli ya kutumia fursa yoyote ya kisiasa na kiuchumi kufaidika na mengi mazuri yaliyoko barani Afrika. Nafasi ya kisiasa na kiuchumi ya Afrika Kusini ni kubwa barani humo na nchi zote duniani zinaiangalia Afrika Kusini kama lango muhimu la kuingilia barani humo. Kuhusiana na suala hilo, Habibollah Ansari, naibu wa mkuu wa Baraza la Ushirikiano wa Kiuchumi la Iran na Afrika amesema hivi karibuni kwamba: Bara la Afrika lina watu bilioni moja na milioni 200 na nchi zote za Afrika zina fursa nzuri ya kustawisha uwekezaji katika masuala ya kibiashara, kiuchumi na mengineyo.
Kwa kuzingatia soko hilo kubwa, serikali ya Iran inalipa umuhimu mkubwa bara la Afrika na bila ya shaka msimamo huo wa kulipa umuhimu bara hilo tajiri kwa maliasili ni wa busara sana. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za Afrika zinaweza kufaidishana sana katika nyuga zote chini ya mwavuli wa ushirikiano wa kiuadilifu na wa kuheshimiana, na huo ndio msimamo wa Tehran katika siasa zake za nje.