Zarif: Iran ni mshirika wa kuaminiwa wa Afrika Kusini
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Iran inaweza kuwa mshirika wa kuaminika wa Afrika Kusini katika eneo la Mashariki ya Kati.
Muhammad Javad Zarif ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Spika wa Bunge la Afrika Kusini, Baleka Mbete aliyeko safarini hapa nchini. Amesema Afrika Kusini imekuwa rafiki wa Iran hususan katika kipindi cha vikwazo na ametoa wito wa kupanuliwa zaidi ushirikiano wa nchi mbili katika nyanja zote hususan ushirikiano wa kibenki.
Kwa upande wake Spika wa Bunge la Afrika Kusini, Baleka Mbete amekaribisha wito wa kuzidishwa uhusiano wa pande mbili na ushirikiano wa kibenki na Iran. Mbete amesema kuwa, nchi mbili za Iran an Afrika Kusini zina uwezo na rasilimali nyingi ambazo zinapaswa kutumiwa kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Spika wa Bunge la Afrika Kusini pia wamezungumzia suala la kuanzishwa kamisheni ya ushirikiano, safari ijayo ya Rais wa Iran nchini Afrika Kusini, makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na hali ya sasa ya Mashariki ya Kati hususan kadhia ya Palestina.