Hija katika mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, jana alikutana na viongozi na wasimamizi wa msafara wa mahujaji wa Iran ambako ameashiria kuwepo kambi hatari sana, amilifu na iliyojizatiti kwa anuwai za nyenzo na suhula za propaganda ya kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amesema kwamba: "Mfumo wa Kiislamu una uwezo na nyenzo nyingi sana za kuuwezesha kusimama kidete kujihami na kuiandama kambi hiyo; na njia ya kukabiliana na kambi hiyo hatari ni utaalamishaji na ulinganiaji amilifu na ya ushambuliaji; na Hija ni moja ya vituo vikuu na vya msingi vya kutekelezea hatua hiyo".
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kuwa kuzifunga au kuziwekea mipaka njia za mawasiliano kati ya Iran na mahujaji wa mataifa mengine, kama dua ya Kumeili, mkusanyiko wa kujibari na kujitenga na washirikina pamoja na mijumuiko na makongamano ya tablighi ni mbinu inayotumiwa na serikali ya Saudi Arabia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na akafafanua kwamba: "Hii leo katika Ulimwengu wa Kiislamu kuna wasomi na wenye vipawa wengi ambao wana hamu ya kusikia ukweli na hakika ya mambo kupitia Jamhuri ya Kiislamu; kwa hivyo inapasa zitumike nyenzo mpya na za kisasa za ulinganiaji na lugha athirifu, maneno mazuri na hoja madhubuti kuwafikishia wakusudiwa ujumbe wa masuala muhimu kama kupambana na ubeberu, kufichua utambulisho halisi wa Magharibi, kujibari na maadui wa Uislamu pamoja na madhumuni na makusudio aali na ya kina yaliyomo kwenye dua ya Kumeili".
Katika dunia iliyojaa machafuko na makelele mengi ya sasa kuna mataifa mengi yenye kiu ya kutaka kujua haki na kweli. Mkabala wa propaganda chafu za mirengo inayoeneza uongo kupitia vyombo vya habari vya Magharibi na vibaraka wao ambao daima wanafanya jitihada za kupotosha ukweli na kuficha haki, kuna kambi mbili. Kambi ya kwanza ni ile ya shakhsia wanaojitoa mhanga na wenye moyo wa kufa shahidi kwa ajili ya kulinda haki, kweli na hakika. Mfano wa kambi hiyo ni vijana wa Kiislamu kama Shahidi Muhsin Hojaji wanaoendelea kutoa roho zao kwa ajili ya kulinda Uislamu na matukufu yake.
Muhsin Hojaji ambaye alikuwa miongozi wa vijana waliokwenda Iraq na Syria kulinda haram za watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw) mbele ya hujuma za makundi ya kiwahabi na kitakfiri, aliuawa shahidi tarehe 9 Agosti mwaka huu baada ya kukamatwa mateka na kundi la kigaidi la Daesh katika mpaka wa Syria na Iraq. Moyo kama huu wa kimapinduzi na kuwa tayari kufa shahidi kwa ajili ya Uislamu na matukufu yake, ndivyo vinavyowatia wahka na woga mkubwa maadui wa Uislamu.
Wenzo wa pili yenye taathira kubwa katika kufikisha ujumbe wa haki wa Uislamu kwa walimwengu ni kuweka wazi uhalisia wa mambo na kufichua utambulisho halisi wa mabeberu. Jukumu hizo kubwa linaweza kutekelezwa vyema zaidi katika baadhi ya vipindi na misanaba kuliko nyakati nyinginezo. Ni kutokana na ukweli huo ndipo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei akasema: "Fursa ya Hija ni minbari bora zaidi ya ulinganiaji kwa ajili ya kujenga mawasiliano na walimwengu na kuzima propaganda za upande wa pili".

Miongoni mwa vitisho vikubwa vinavyoukabili Umma wa Kiislamu na matukufu yake kwa sasa ni mifarakano na ukatili unaofanyika kwa jila la Uislamu. Hapana shaka kuwa, kutangaza tajiriba na uzoefu wa Iran kwa mataifa mengine wakati wa msimu wa ibada ya Hija kunaweza kusaidia juhudi za kuzima na kubatilisha njama na hatari hizo. Kuhusu suala hilo Ayatullah Khamenei amesema: "Wakati wa msimu wa Hija, viongozi wa Saudia walijitokeza bila aibu wala haya katika televisheni na kuzungumza dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na ni kawaida kwamba maneno hayo yatazusha shaka na utata kwa watu wa kawaida katika nchi nyenginezo, lakini kinachopasa kufanywa ni kuwa na mawasiliano na watu ili kuondoa shaka na utata na kuuvunja mzingiro uliowekwa na upande wa pili".