Oct 16, 2017 02:32 UTC
  • Larijani: Marekani haiheshimu mapatano ya kimataifa

Spika wa Bunge la Iran Ali Larijani amesema Rais Donald Trump wa Marekani hajali mapatano ya kimataifa na wala haheshimu Umoja wa Mataifa na amezionyesha nchi zote kuwa nchi yake haiminiki.

Larijani aliyasema hayo jana Jumapili mjini Saint Petersburg nchini Russia wakati akihutubia mkutano wa 137 wa Jumuyia ya Kimataifa ya Mabunge. Ameongeza kuwa, matamshi yaliyojaa chuki ya Rais Trump wa Marekani dhidi ya Iran ni kielelezo cha kutoaminika tena Washington. Spika Larijani amesema mara kadhaa Marekani imekuwa ikiingilia mambo ya ndani ya Iran na mfano wa wazi ni hatua yake ya kushiriki katika kuiangusha serikali ya kisheria ya Iran mwaka 1953, kujaribu kuiangusha serikali ya Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kuunga mkono utawala wa Baath wa Iraq katika vita vyake vya miaka minane dhidi ya Iran na kuitungua ndege ya abiria ya Iran katika Ghuba ya Uajemi mwaka 1988.

Mkutano wa 137 wa Jumuyia ya Kimataifa ya Mabunge

Larijani amesema, tuhuma za Trump dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH zinatolewa katika fremu ya mkakati wa Marekani ya kuunga mkono kundi la kigaidi la ISIS yaani Daesh. Amesema Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limezisaidia  Iraq na Syria katika vita dhidi ya kundi la kigaidi la ISIS kufuatia ombi la serikali za nchi hizo mbili za Kiarabu. Amesema ni jambo la kushangaza kuona kuwa baada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi  kufanikiwa kukabiliana na ISIS, sasa Marekani inadai jeshi hilo eti linaunga mkono ugaidi.

Aidha amesema hatua ya Marekani kuzitaja harakati za Hizbullah ya Lebanon na Hamas ya Palestina kuwa eti ni makundi ya kigaidi haiwezi kupunguza thamani za makundi hayo. Amesema makundi hayo mawili yanahusika katika mapambano halali dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Tags