Tehran: Israel, US hazina ufahamu juu ya taifa la Iran
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema utawala wa Kizayuni wa Israel, Marekani na nchi nyingine zinazojifanya kutetea haki za Wairani hazina ufahamu wowote kuhusu taifa la Iran.
Abdolreza Rahmani Fazli amesema, na hapa tunanukuu: "Maadui zetu ambao wenyewe hawana msimamo katika nchi zao na wala hawajachaguliwa na wananchi, katika siku chache zilizopita wanajifanya kuwaunga mkono wananchi wa Iran na kuwa mstari wa mbele kutetea haki zao."
Amesema utawala ghasibu wa Israel, nchi ya kibeberu ya Marekani na tawala zingine za eneo zinajifanya kutoa radiamali za haraka kuonyesha kuwa wanaliunga mkono taifa la Iran, ilhali siku zote hazijawahi kuwatambua Wairani.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema maadui wa taifa hili wamejenga taswira mbovu kwenye akili zao na kutaka kutumia vibaya maandamano ya amani ya Wairani.
Amebainisha kuwa, kuwa macho wananchi wa Iran bila shaka kutatibua njama za maadui wasioitakia mema nchi hii na wanaotaka kueneza machafuko na taharuki.
Afisa huyo wa ngazi za juu wa Iran amesema mihimili yote ya serikali inafuatilia kwa karibu malalamiko ya wananchi ili kuyatafutia ufumbuzi.