Iran kuishtaki Marekani kwa kutumia ushahidi wa Trump
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajiandaa kuishtaki Marekani kwa kushiriki kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika mashambulizi ya kigaidi ya mwaka jana hapa nchini, kwa kutumia ushahidi wa Rais Donald Trump.
Abolfazl Aboutorabi, mwanachama wa Kamati ya Mahakama ya Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema rais huyo wa Marekani amekuwa akikiri mara kwa mara tena hadharani kwamba nchi yake ndiyo iliyounda kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS), ambalo lilihusika katika mashambulizi pacha hapa nchini mwaka jana.
Amesema, "Wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais huko Marekani mnamo Januari mwaka 2016, Trump aliwaambia wafuasi wake kuwa, Hillary Clinton, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ndiye aliyeasisi kundi la kigaidi la ISIS kutokana na sera zake ghalati."
Afisa huyo wa Bunge la Iran ameongeza kuwa, katika mahojiano ya 'Dakika 60 ya CBS' Trump alisisitiza kuwa, Hillary Clinton ndiye muasisi wa kundi la kigaidi la ISIS, na alichukua hatua hiyo kutokana na sera zake mbovu za mambo ya nje.
Mwanachama huyo wa Kamati ya Mahakama ya Bunge la Iran ameongeza kuwa, Iran itatumia ushahidi huo wa maneno ya Trump kuishtaki Washington katika Mahakama ya Kimataifa, na kuibebesha dhima ya damu za Wairani waliouawa katika mashambulizi hayo ya mwaka jana.
Itakumbukwa kuwa, Juni 7 mwaka jana, wananchi 17 wa Iran waliuawa shahidi, huku makumi ya wengine wakijeruhiwa, kufuatia mashambulizi ya bomu na risasi dhidi ya Bunge la Iran na Haram ya Muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, Ayatullah Khomeini MA hapa mjini Tehran.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) liliituhumu Saudi Arabia kuwa ndiyo iliyopanga hujuma hiyo, kwa kuzingatia kuwa ilifanyika wiki moja baada ya Trump kukutana na watawala wa Riyadh wanaounga mkono ugaidi.