Rais Rouhani awatumia Waislamu mkono wa Idi
(last modified Thu, 14 Jun 2018 15:55:29 GMT )
Jun 14, 2018 15:55 UTC
  • Rais Rouhani awatumia Waislamu mkono wa Idi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewatumia mkono wa Idi viongozi wa nchi za Kiislamu na Waislamu wote kwa mnasaba wa kukaribia kuingia katika sikukuu ya Idul Fitr.

Jioni ya leo Alkhamisi, Rais Hassan Rouhani amewatumia mkono wa Idi viongozi hao na kusema: Kwa baraka za sikukuu iliyojaa baraka na rehema na chini ya kivuli cha kutii amri za Mwenyezi Mungu ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, ni matarajio yangu kuwa umma wote wa Kiislamu utakuwa umepata unyofu na usafi wa nyoyo na matendo katika mwezi huu na kila mmoja wetu atajitahidi kadiri inavyowezekana kujiidilisha kubakia katika njia tukufu ya kufikia kwenye ukamilifu wake wa kibinadamu. 

Sala ya Idul Fitr ya mamia ya maelfu ya Waislamu nchini Bangladesh

 

Rais Rouhani aidha amesisitiza kuwa, ni matumaini yangu umma wa Kiislamu utaweza kutumia vizuri mafundisho ya kijamii yanayopatikana katika sikukuu hii azizi na tutaweza kushuhudia mshikamano na mfungamano zaidi wa Waislamu katika kupambana na machafuko na misimamo ya kuchupa mipaka. Ni matumaini yangu tutaweza kuitumia vizuri sikukuu hii kuleta umoja na wahda baina ya Waislamu katika kukabiliana na siasa za mabeberu wa dunia wasio na mwamana na wanaojikumbizia kila kitu upande wao, kama ambavyo ni matarajio yangu umoja na mshikamano huo wa Waislamu utaweza kuleta amani na utulivu katika kona zote za dunia.

Katika sehemu ya mwisho ya ujumbe wake huo, Dk Rouhani amemuomba Mwenyezi Mungu Mtukukfu kulinda heshima na ufanisi wa Waislamu wote duniani.

Sehemu kubwa ya nchi za Kiislamu duniani zinatarajia kusherehekea sikukuu ya Idul Fitr ya mwaka huu wa 1439 Hijria, kesho Ijumaa Juni 15, 2018 tukijaaliwa. 

Tags