Jul 03, 2018 04:55 UTC
  • Ayatullah Amoli Larijani: Ni Jukumu la Waislamu kuonyesha sura khabithi ya Marekani

Mkuu wa Vyombo vya Mahakama nchini Iran ameashiria jinai za Marekani nchini Iran na Yemen na kujitoa serikali ya Rais Donald Trump katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kusema kuwa, hatua za serikali ya Washington ni za kibabe.

Ayatullah Amoli Larijani amebainisha kwamba, hatua za Marekani ambayo ni mtenda jinai si za kiutu hata kidogo na inashangaza wakati huo huo, Washington bila hata haya inazituhumu nchi nyingine kwamba, zinakiuka haki za binadamu.

Mkuu wa Vyombo vya Mahakama nchini Iran amesisitiza juu ya udharura wa kukabiliana na jinai za Marekani na kubainisha kwamba, kuionyesha sura khabithi ya Marekkani ni jukumu la Waislamu wote na nchi za Kiislamu na kwamba, haipaswi kuomba msaada kwa nchi zinazotenda jinai ambazo zinadai kutetea haki za binadamu ulimwenguni.

Ayatullah Amoli Larijani (kushoto) akiwa na Rais Hassan Rouhani pamoja na Spika Ali Larijani

Ayatullah Amoli Larijani amesema kuwa, kuwatenganisha watoto wahajiri 2,500 na wazazi wao huko Marekani, ni hatua ambayo haioani kabisa na kigezo chochote kile cha ubinadamu na haki za binadamu.

Kadhalika Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Jamhuri ya Iran ameongeza kuwa, hata kama wazazi wa watoto hao watakuwa ni wahalifu, lakini kitendo cha kuwatenganisha watoto wadogo na wazazi wao hakiwezi kuhalilishwa kwa namna yoyote ile.

Amesema kuwa, hatua hizo za Marekani ni sehemu inayoweka wazi jinsi suala la haki za binadamu lilivyo nchini Marekani.

Tags