Rais Rouhani: Iran haiiamini Marekani hata kidogo
Rais Hassan Rouhani amesema Iran haiiamini Marekani hata kidogo na kwamba nchi za Ulaya, China na Canada, nazo pia hazina imani tena na nchi hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sekta ya Ulinzi nchini na kuongeza kuwa: wabunge wa Kongresi ya Marekani wamepitisha sheria inayotaka nchi hiyo ihakikishe haiingii vitani na Iran kwa sababu wanajua kwamba Iran ina nguvu na uwezo, na kuishambulia Iran kutaigharimu Marekani.
Huku akisisitiza kwamba utayarifu wa vikosi vya ulinzi inapasa ufikie kiwango cha kumfanya adui asithubutu kuanzisha uchokozi, Rais Rouhani amebainisha kuwa: Juhudi inazofanya na gharama zote inazogharimika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa kiulinzi ni kwa lengo la kuzuia isivamiwe na kulazimishwa kupigana vita vyenye gharama kubwa.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: taifa la Iran siku zote limekuwa likiishi kwa amani na masikilizano na maelewano na nchi nyingine; na maana ya kujizatiti kiulinzi ni kuweza kuwa na amani endelevu. Ameongeza kuwa kutokuwa na utayarifu na uwezo wa kutosha wa kujihami, maana yake ni kukaribisha vita na kutoa baraka kwa adui za kuivamia nchi.
Rais Rouhani ameashiria pia baadhi ya nchi jirani ambazo kidhahiri zinafanya jitihada za kiulinzi kwa ajili ya kulinda usalama wao na kueleza kwamba: wao wananunua silaha wa bei kubwa kabisa lakini ili kuweza kuzitumia silaha hizo wanalazimika kutii matakwa ya wauzaji wake.
Leo tarehe 21 Agosti ni Siku ya Sekta ya Ulinzi nchini Iran.../