Iran: Trump ni mwanagenzi wa hali ya Mashariki ya Kati
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, rais wa Marekani, Donald Trump ni mwanagenzi na hana welewa wa kutosha kuhusu hali ya Mashariki ya Kati wala historia, sifa maalumu za watu wake na pia matukio ya miaka ya hivi karibuni ya eneo hili.
Bahram Qassemi alisema hayo jana Ijumaa wakati alipohojiwa na shirika la habari la wanafunzi wa vyuo vikuu la ISNA na kubainisha kuwa, inasikitisha kuona kwamba washauri wakubwa wa Donald Trump wanampotosha na kumpa taarifa zisizo sahihi ambazo wanazikusanya kutoka kwa magenge ya kigaidi ambayo yanataka Marekani ijiingize muda wote katika masuala ya Mashariki ya Kati na matokeo yake ni kuzidi kumchafua Trump na manufaa ya watu wa Marekani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran vile vile amegusia matamshi ya hivi karibuni ya Trump kuhusu Iran wakati alipohojiwa na gazeti la Marekani la Wall Street Journal na kuongeza kuwa, inasikitisha kuona kwamba rais wa Marekani ana mazoea mabaya sana ya kurudia riwaya zile zile za kila siku na zisizo sahihi kuhusu Iran.
Vile vile amejibu madai ya Trump ya kwamba eti kabla ya kuingia kwake katika Ikulu ya Marekani, White House, Iran ilikuwa iko kila sehemu na ilikuwa inayateka maeneo yote kama vile Syria na Yemen na kusema kuwa, katika kipindi cha mamia ya miaka iliyopita, Iran haijawahi hata mara moja kuvamia nchi yoyote wala kuwa na tamaa ya kuchukua hata shibri moja ya nchi nyingine, na Iran haikuwa imeteka eneo lolote lile hata kabla ya kuingia madarakani Donald Trump huko Marekani.
Amesema, siasa za kimsingi na zisizobadilika za Iran ni kupiga vita misimamo mikali na ugaidi na kufanya juhudi za kuleta amani, umoja na utulivu katika eneo hili, suala ambalo linawachukiza wale wote wanaolitakia mabaya eneo la Mashariki ya Kati.