Iran imejitosheleza katika sekta ya kujihami majini
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49799-iran_imejitosheleza_katika_sekta_ya_kujihami_majini
Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema leo kwamba nchi hii imejitosheleza katika sekta ya kujihami majini ikiwa ni pamoja na kujitegeneza zana za juu na chini ya maji.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Nov 27, 2018 11:29 UTC
  • Iran imejitosheleza katika sekta ya kujihami majini

Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema leo kwamba nchi hii imejitosheleza katika sekta ya kujihami majini ikiwa ni pamoja na kujitegeneza zana za juu na chini ya maji.

Admeri Hossein Khanzadi aliyesema hayo leo Jumanne mjini Tehran akiwa ameandamana na makamanda wengine wa jeshi hilo walipozuru Haram ya Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa lengo la kumsomea al Fatiha na kutangaza tena kuendelea kuwa watiifu kwa malengo yake matakatifu. Admeri Khanzadi amesema kujitosheleza Iran katika sekta ya kihijami majini ni jambo linaloashiria kuwa, vikwazo havijaweza kuwa na athari hasi.

Aidha ameashiria mafanikio ya wataalamu wa ndani ya Iran katika kuunda meli ya kisasa ya kivita iliyopewa jina la Jamaran miaka 10 iliyopita na kusema: "Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, zana za kivita za Jeshi la Majini zimekuwa zikundwa hapa nchini." Amesema hivi sasa manoari za Iran zinalinda doria katika maji ya kimataifa.

Meli ya kivita ya Jamaran iliyoundwa na wataalamu Wairani bila kutegemea msaada wa kigeni

Kesho Novemba 28 ni Siku ya Kitaifa ya Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na maadhimisho ya hamasa iliyoibuliwa na mabahari ya manowari ya kuvurumisha makombora ya Peykan.

Katika siku kama hii miaka 38 iliyopita, vikosi vya Jeshi la Majini la Iran vilifanya operesheni katika maji ya Ghuba ya Uajemi na kufanikiwa kuvisambaratisha vikosi vya majini vya jeshi la Iraq. Tukio hilo lilitokea takribani miezi miwili tu baada ya kuanza vita vya kichokozi vya Iraq dhidi ya Iran. Operesheni hiyo ilipelekea kutokea mapigano makali kati ya meli za kivita za pande mbili na meli nyingi za kivita za Iraq ziliteketezwa. Kutokana na ushujaa wa wapiganaji wa vikosi vya majini katika operesheni hiyo, siku hii inajulikana hapa nchini kwa jina la “Siku ya Jeshi la Majini”.