Maonyesho ya Ndege yafanyika Kish, Iran
Maonyesho ya 9 ya Ndege ya Iran yanaendelea katika kisiwa cha Kish kusini mwa Iran katika Ghuba ya Uajemi licha ya vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Maonyesho hayo ya siku nne yalianza Jumatatu na yanashirikisha mashirika 105 ya Iran na 10 ya kigeni.
Katibu wa maonyesho hayo, Bijan Bonakdar amesema kuwa, washiriki wanaonyesha mafanikio yao ya hivi karibuni katika sekta ya usafiri wa anga wakati huu ambao Marekani inazishinikiza nchi zingine ziunge mkono vikwazo vyake dhidi ya Iran.
Maonyesho hayo ambayo yalifunguliwa rasmi na Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Amir Hatami ni tukio muhimu zaidi katika sekta ya usafiri wa anga nchini Iran na hufanyika mara moja kila baada ya miaka miwili.
Akizungumza Jumatatu wakati wa ufunguzi wa maonyesho hayo, Brigedia Jenerali Abdolkarim Banitarafi, Mkuu wa Shirika la Viwanda vya Usafiri wa Anga Iran alisema Iran iko tayari kuuza ndege zake za kivita zilizoundwa hapa nchini katika soko la kimataifa. Amesema Iran tayari imeshaanzisha mkakati wa kuuza ndege zake za kivita katika soko la kimataifa.
Hivi karibuni Iran ilizindua ndege ya kivita iliyotegenezwa kikamilifu hapa nchini na iliyopewa jina la 'Kowsar'. Weledi wa mambo wanaamini kuwa kufanyika maonyesho hayo ni ishara kuwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vimefeli.