Ayatullah Siddiqi: Demokrasia ya Uliberali imefika ukingoni
Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran amesema demokrasia ya uliberali duniani ipo ukingoni kusambaratika na kutoweka kikamilifu.
Hujjatul Islam wal Muslimin Kadhim Siddiqi ameashiria maandamano ya 'Vizibao vya Njano' nchini Ufaransa na katika baadhi ya nyingine za Ulaya na kubainisha kuwa, uliberali ambao umewahadaa walimwengu kwa karibu karne moja sasa umefikia tamati.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran amebainisha kuwa, njama za Rais Donald Trump wa Marekani za kujaribu kuchochea machafuko na ghasia hapa nchini kupitia vikwazo na mashinikizo ya kifedha zimegonga mwamba.
Amesema njama hizo ambazo Trump alizipa jina la 'Joto Kali Kwenye Msimu wa Joto' hazikufua dafu, kwani wananchi Waislamu wa Iran licha ya vikwazo na mashinikizo lakini walikuwa na wakati mzuri katika msimu wa joto.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake hii leo hapa mjini Tehran, Hujjatul Islam wal Muslimin Kadhim Siddiqi amewatahadharisha maofisa wa serikali hapa nchini, kusaini miswada ya Shirikisho la Kupambana na Fedha Chafu na Ufadhili wa Makundi ya Kigaidi (FATF), akisisitiza kwamba iwapo vyombo vya dola vinataka kupambana kwa dhati na utakatishaji wa fedha chafu na ufadhili wa makundi ya kigaidi, basi watumie sheria za hapa nchini.
Amesema kusaini miswada hiyo ya (Financial Action Task Force) ni sawa na kuanzisha mchakato wa kujiwekea vikwazo, akisisitiza kuwa, tayari taifa hili lina uzoefu wa kutoheshimiwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na kwa msingi huo Iran haipaswi tena kuyaamini madola ajinabi.