Mtangazaji wa Press TV, Bi. Hashemi, kufikishwa mahakamani Marekani
Mtangazaji wa Televisheni ya Press TV, Bi. Marzieh Hashemi, ambaye amekuwa akishikiliwa kwa siku kadhaa na polisi ya Marekani, FBI, bila kufahamishwa sababu za kukamatwa kwake anatazamiwa kufikishwa mahakamani mjini Washington DC leo Ijumaa.
Imearifiwa kuwa, Bi.Hashemi, ambaye ni raia wa Marekani anayefanya kazi nchini Iran, amekamatwa kwa ajili ya kutoa ushahidi katika kesi ya jinai. Hayo yamedokezwa na mwanae Bw. Hussein Hashemi ambaye anasema mama yake alikuwa amefika Marekani kutembelea familia na kutengeneza filamu kuhusu maisha ya Wamarekani wenye asili ya Afrika ambao wanakandamizwa na utawala wa Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amelaani kukamatwa Bi. Hashemi na kutaja kitendo hicho kuwa ni 'mchezo wa kisiasa'. Ametaka wakuu wa Marekani wamueachilie huru mara moja. Zarif amesema kwa kuzingatia kuwa mume wa Bi. Hashemi ni Muirani, anatambuliwa kama raia wa Iran pia na ni jukumu la Iran kutetea raia wake.
Bi Hashemi, Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika, aliyekuwa akiitwa Melanie Franklin kabla ya kusilimu alitiwa nguvuni Jumapili St. Louis, Missouri na kupelekwa mjini Washington DC ambako amewekwa kizuizini tokea Jumapili bila ya kuelezwa amekamatwa kwa kosa gani.
Mkuu wa Kitengo cha Kimataifa cha IRIB Dkt. Peyman Jebeli amesema, "Hakuna sababu yoyote ya kukamatwa Marzieh Hashemi nchini Marekani. Kosa lake kubwa ni kuwa yeye ni mwanamke Mwislamu Mmarekani na tokea mwaka 2003 amekuwa akifanya kazi na Press TV."
Ameashiria namna wakuu wa Marekani wanavyomdhalilisha Marzieh Hashemi akiwa korokoroni ikiwa ni pamoja na kumvua hijabu yake na kumlazimisha ale nyama ya nguruwe ambayo ni haramu kwa Waislamu na kusema, kitendo hicho ni ukiukwaji wa wazi wa matukufu na thamani za Kiislamu. Aidha amesema mbali na kumnyima chakula cha halali, wakuu wa Marekani pia wamekataa kumpa Bi. Hashemi nguo zinazofaa katika msimu huu wa baridi kali nchini humo.