Salehi: Iran itaendelea na miradi yake ya nyuklia kwa nguvu zake zote
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i51064-salehi_iran_itaendelea_na_miradi_yake_ya_nyuklia_kwa_nguvu_zake_zote
Mkuu wa taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea na miradi yake ya nyuklia katika nyuga za utafiti, uvumbuzi, urutubishaji urani, ujenzi wa vinu na mashinepewa (centrifuge) mpya kwa nguvu zake zote.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 23, 2019 04:26 UTC
  • Salehi: Iran itaendelea na miradi yake ya nyuklia kwa nguvu zake zote

Mkuu wa taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea na miradi yake ya nyuklia katika nyuga za utafiti, uvumbuzi, urutubishaji urani, ujenzi wa vinu na mashinepewa (centrifuge) mpya kwa nguvu zake zote.

Dk Ali Akbar Salehi amesema hayo usiku wa kuamkia leo katika mahojiano aliyofanyiwa na Kanali ya Nne ya televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa, suala la kiufundi katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA limewekwa kwa namna ambayo linaiwezesha Iran kuendelea na utafiti wake katika masuala ya nyuklia bila ya kuvunja vipengee vya mapatano hayo.

Vile vile amesema, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu hakuruhusu miradi ya nyuklia ya Iran isimame kwa sababu ya makubaliano ya JCPOA. Amesisitiza kuwa, Iran imeweza kupiga hatua nzuri za kimaendeleo katika urutubishaji urani baada ya kutolewa amri na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya kuendelea na urutubishaji huo kwa kiwango cha SEW laki moja na 90 elfu.

Keki ya njano ya urani

 

Mkuu huyo wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran ameongeza kuwa, katika kipindi cha takriban siku kumi zijazo, tani 30 za keki ya njano ya nyuklia zitapelekewa Isfahan, (katikati ya Iran).

Salehi amegusia pia uamuzi wa Marekani wa kutoheshimu ahadi zake na kujitoa katika mapatano ya JCPOA na kusema kuwa, Marekani inatumia mabavu kuzitisha nchi nyingine, lakini nchi za dunia haziamini kwamba Washington inaweza kufanikiwa kuyashinikiza mataifa yote kwa kutumia nguvu.

Itakumbukwa kuwa tarehe 4 Juni 2018 kwenye kumbukumbu za mwaka wa 29 wa kufariki dunia Imam Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliwapa jukumu viongozi na maafisa wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran kuhakikisha kwamba wanaongeza kasi ya kufikia haraka kiwango cha SEW laki moja na 90 elfu za ututubishaji urani kwa mujibu wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA.