Zarif: Iran haitazisubiri nchi za Ulaya katika mabadilishano ya kifedha
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i51343-zarif_iran_haitazisubiri_nchi_za_ulaya_katika_mabadilishano_ya_kifedha
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema katika suala la mabadilishano ya kifedha, Iran haitazisubiri nchi za Ulaya. Aidha amesisitiza kuwa, mfumo uliozinduliwa wa kuunga mkono mabadilishano ya kibiashara kati ya Iran na Ulaya ni wa majaribio na inasubiriwa kuona ni vipi nchi za Ulaya zinalipa uzito suala hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 05, 2019 01:16 UTC
  • Zarif: Iran haitazisubiri nchi za Ulaya katika mabadilishano ya kifedha

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema katika suala la mabadilishano ya kifedha, Iran haitazisubiri nchi za Ulaya. Aidha amesisitiza kuwa, mfumo uliozinduliwa wa kuunga mkono mabadilishano ya kibiashara kati ya Iran na Ulaya ni wa majaribio na inasubiriwa kuona ni vipi nchi za Ulaya zinalipa uzito suala hilo.

Akizungumza Jumatatu baada ya kushiriki katika kikao cha Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni katika Bunge la Iran, Zarif alisema: "Hatua ya nchi za Ulaya kuanzisha mfumo wa kifedha na mabadilishano ya kibiashara na Iran imefanyika kwa kuchelewa na ilipaswa kutekelezwa mapema." Amesema uanzishwaji wa mfumo huo ulicheleweshwa na nchi za Ulaya kutokana na mashinikizo ya Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema nchi za Ulaya zingepaswa kuanza kutekeleza ahadi zao mapema zaidi na kuongeza kuwa: "Iran imetekeleza ahadi zake zote katika fremu ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA lakini nchi za Ulaya hazijatekeleza ahadi zao na hazijafidia hatua ya Marekani kujiondoa JCPOA."

Zarif aidha amesema Mfumo wa Kuunga Mkono Mabadilishano ya Kibiashara ambao kwa Kiingereza unajulikana kama Instrument in Support of Trade Exchanges (INSTEX) ni muhimu kwa Ulaya zaidi kuliko Iran kwani utaweza kuonyesha kuwa Umoja wa Ulaya unaweza kuchukua maamuzi huru.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa mfumo huo utawezesha kuwepo mabadilishoano ya kifedha kati ya nchi 28 za Umoja wa Ulaya na utahusu bidhaa ambazo hazijawekewa vikwazo lakini wigo huo utapanuliwa baadaye.

Ikumbukwe kuwa, Januari 31  nchi za Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zilianzisha mfumo maalumu wa kifedha usiotumia sarafu ya dola kwa ajili ya kurahisisha mabadilishano ya kibiashara na kiuchumi na Iran na wakati huohuo kukwepa vikwazo vya Marekani.